Pages

Monday 25 August 2014

Wanaopeleka kortini Bunge la Katiba waongezeka


Mwandishi wa habari,Said Kubenea.

Idadi ya raia wanaohoji mahakamani uhalali wa Bunge Maalum la Katiba kuendelea kujadili Rasimu ya Katiba mpya imezidi kuongezeka.

Baada ya mwandishi wa habari, Said Kubenea kufungua kesi kuhoji uhalali wa Bunge hilo wiki iliyopita, Mjumbe wa Bunge hilo, Said Arfi (Chadema), naye ametangaza kuwa anakusudia kwenda mahakamani kufungua kesi ili kupata ufafanuzi wa mahakama juu ya uhalali wa bunge hilo kuacha kujadili Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Wiki iliopita, Kubenea alifungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupitia kwa Wakili wake, Peter Kibatala dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).Katika kesi hiyo Namba 28 ya mwaka 2014, Kubenea anaiomba mahakama itoe tafsiri sahihi ya Mamlaka ya Bunge la Katiba.

Kubenea alifungua kesi hiyo akiiomba Mahakama itoe tafsiri hiyo chini ya vifungu vya 25 (1) na 25(2) vya Sheria ya Marekebisho ya Katiba Namba 83 ya mwaka 2011.

Sambamba na kesi hiyo ya kuomba tafsiri ya mamlaka ya Bunge hilo, pia amewasilisha maombi mahakamani hapo akiiomba mahakama itoe zuio la muda la kusimamisha Bunge hilo ili kusubiri uamuzi wa maombi ya tafsiri hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Arfi mjini Dodoma jana, anakusudia kwenda mahakamani kupinga kuendelea kwa Bunge Maalum la Katiba kwa sababu kinachoendelea kwa sasa ni kamati mbalimbali kuendelea kujadili rasimu ya CCM badala ya ile iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.

“Kutokana na vikao vinavyoendelea, kinachoonekana siyo kutengeneza katiba mpya bali ni kufanya marekebisho makubwa katika katiba iliyopo na hilo limeisaidia sana CCM kutokana na wajumbe wa Ukawa kususia Bunge,” alisema Arfi katika taarifa yake kwa vyombo vya habari na kuongeza:

“Kwa kuwa wabunge wa CCM wamedhamiria kuendelea na mchakato huu kwa kuifanyia marekebisho katiba ya sasa na kuachana na Rasimu ya Jaji Warioba na kwa kuwa hakuna namna ya kuwazuia kufanya hivi baada ya wabunge wa Ukawa kususa, mimi nakusudia kuchukua hatua za kisheria kwenda mahakamani ili kupata ufafanuzi wa mahakama juu ya uhalali wa Bunge Maalum la Katiba kuacha Rasimu ya Tume.”

Alisema anawasiliana na wanasheria wake na mchakato unaendelea ili kesi hiyo ifunguliwe mapema katika hali ya dharura.

Alisema kilichomsukuma kufungua kesi hiyo ni baada ya kuona kuna mambo makubwa mawili yameanzishwa ili kujaribu kuwashawishi Wazanzibari kuendelea kuwa sehemu ya Muungano wa serikali mbili na kuyataja kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa makamu watatu wa Rais yaani Makamu wa Rais (Mgombea Mwenza), Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu.

“Kimsingi tunarudi kule kule walikopendekeza Tume kwa sababu ukichambua pendekezo hili unakutana na serikali tatu ambazo ni Tume imependekeza,” alisema.

Alitaja jambo lingine kuwa ni kuanzishwa kwa mabunge matatu ambayo ni ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zanzibar na Tanganyika.

“Ukichambua pendekezo hili unakutana na serikali tatu kwa sababu huwezi kuwa na Bunge la Tanganyika bila kuwa na serikali kwa sababu kazi kubwa ya Bunge ni pamoja na kuisimamia serikali,” alisema.

Aidha, alisema pamoja na hayo yote pia kuna mambo mazuri ambayo yameingizwa kwenye Rasimu hiyo yakiwamo haki za wakulima, wafugaji na wavuvi kumiliki ardhi, haki ya afya, chakula, maji safi na salama, haki ya hifadhi ya jamii na haki ya makazi.

Alisema kinachofanyika kwa sasa siyo kutengeneza Katiba mpya bali kufanya marekebisho makubwa katika Katiba iliyopo.

“Hili limewezekana kwa sababu wenzangu wajumbe wa upinzani kususa…tungekuwapo wote ndani ya Bunge hili lisingewezekana kwa sababu tungepinga kwa nguvu zaidi na hata kuhakikisha Bunge haliendelei…kwa kuwa wabunge wa CCM wamedhamiria kuendelea na mchakato huu wa kuifanyia marekebisho ya Katiba ya sasa na kuachana na Rasimu ya Warioba,” alisema.

Mbali na Arfi na Kubenea, Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP) ambaye pia ni mjumbe wa Bunge hilo, Mchungaji Christopher Mtikila, amesema atafungua kesi kama hiyo wiki hii huku Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kikisema kinajiandaa pia kwenda mahakamani kuomba tafsiri hiyo.

Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi ulisusia Bunge hilo Aprili 16, mwaka huu pamoja na mambo mengine, kulalamikia Bunge hilo kuweka kando Rasimu ya Tume na kujadili rasimu ya CCM.

Kujitoa kwa wajumbe wa Ukawa kumesababisha makundi kadhaa ya kijamii kupaza sauti yakitaka Bunge Maalum liahirishwe hadi yatakapopatikana maridhiano ili Katiba iandikwe na makundi yote badala ya chama kimoja.

Hata hivyo, wiki iliyopita, Kamati Kuu ya CCM ilibariki mchakato huo uendelee huku maridhiano yakiendelea kutafutwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

 

Blogger news

Blogroll

LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZA KILA WAKATI

Receive all updates via Facebook. Just Click the Like Button Below

Powered By Blogger Widgets