Pages

Thursday 20 November 2014

SWAGA ZILIKUWA ZAMANI BWANA, KUNA SWAGA SIKU HIZI?

Mandeleo yameua swaga nakwambia. Watu siku hizi wanajidaiii eti wana swaaga, aa wapi!! swaga zilikuwa zamani bwana. Enzi hizo za redio moja, mtu ukitoka kijijini na kuweza kuja kukaa mjini hata wiki moja tu, ukirudi unajikuta wewe ndie mjanja wa kijijini, na kama ulibahatika kuja jiji la Dar es Salaam, basi
watu wote wanakusikiliza wewe unavyowahadithia jinsi ulivyopanda basi la ghorofa, au hata ulivyoibiwa mara baada ya kushuka kituo cha basi, na kila anaetaka kusafiri anakutafuta kukuomba ushauri jinsi ya kujilinda na wezi Dar es salaam.
Swaga zilikuwa enzi hizo ambapo mtu unakuwa ndie mwanafunzi pekee aliyevaa viatu shule nzima, walimu wenyewe wanakuogopa maana lazima wazazi wako wana uwezo mkubwa. Hizo ndio zilikuwa swaga bwana. Kila asubuhi kulikuwa na ukaguzi wa wanafunzi, mwalimu anakagua kucha, meno na lazima kila mtu aonyeshe mswaki wake, swaga ni pale wanafunzi watatu tu shule nzima ndio mna miswaki ya plastiki wengine wote wana miswaki ya miti, hapo utakuta mwalimu mkuu anawatoa mbele na kuonyesha miswaki yenu kwa wengine kama mfano na kuwambia shule nzima, “What is this? This is a toothbrush, haya semeni wote toothbrush” , acha bwana.
Enzi ya Mwalimu hali ilikuwa ngumu , mtu ukiwa na ndugu yako yuko nje, tulikuita Mamtoni, akakuletea suruali ya jeans basi wewe unaweza kuoa chaguo lako, na mji wote wanakutambua kuwa una jeans, enzi hizo kinaitwa ‘kigozi’. Ukiwa na raba zilizoitwa ‘rabamtoni’, au baadae ‘za kuchumpa’ mtaa mzima wanazijua hizo raba sio siku hizi kila nyumba watu wana raba, hakuna swaga bwana siku hizi swaga zamani ndugu yangu.
Watu wengine hawajui kulikuwa na wakati kuwa na TV ilikuwa uhujumu uchumi, hivyo kuwa na TV ilikuwa boooonge ya swaga, japo kulikuwa hakuna kituo cha TV cha kurusha matangazo, TV ilikuwa inaenda na video kaseti, basi kwenu mkiwa na TV, washamba washamba wote wa mtaa unawakaribisha washangae wakati unatafuta mita, TV za siku hizo zilikuwa hazina rimoti, hivyo kuna kigudumu unazungusha hicho hata nusu saa ndipo unaanza kupata picha au sauti , lazima uzungushe mpaka sauti na picha zitokee pamoja, washamba lazima wabaki wanakodoa macho kukuangalia unapofanya maufundi hayo, na baadae kwenda kuhadithiana kwao..
Swaga ilikuwa pale kwenu tu ndio kuna simu mtaa mzima, watu wanakuja kubembeleza simu zao zifikie kwenu na wanalipa wakitaka kupiga kwa ndugu zao, watu walikuwa wakipiga magoti wakati wanaongea na wakubwa zao kwenye simu, na watu wote wanajua mna simu maana waya ya simu ilikuwa ikionekana inaingia kwenu.
Swaga zamani bwana, baba yako akinunua VW hata kama mko watoto wanane na mama yenu na hauzgelo juu mnajazana kwenye kivokswagen kwa starehe kabisa na mzee anazunguka mitaa yote mjini washamba wanawaangalia.
Hizo ndo swaga bwana.
Nakumbuka swaga za mwalimu wangu wa hesabu aliyekuwa anavaa kaptura nyeupe shati jeupe, saspenda nyeusi zimeshikilia kaptura, soksi ndefu zimefika chini ya magoti, viatu vya ngozi vyekundu. Kwenye soksi alikuwa anachomeka kiko na peni aina ya BIC mbili . Kwenye mfuko wa shati peni tatu, mkono wa kushoto ana leso nyeupe, mkono wa kulia ameshika kiboko.
Swaga zilikuwa zamani bwana

No comments:

Post a Comment

 

Blogger news

Blogroll

LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZA KILA WAKATI

Receive all updates via Facebook. Just Click the Like Button Below

Powered By Blogger Widgets