Pages

Friday, 12 December 2014

Lwakatare wa Chadema, Ludovick waibwaga Serikali mahakamani

Dar es Salaam.
Mahakama ya Rufani imetupilia mbali maombi ya marejeo kuhusu uhalali wa uamuzi wa Mahakama Kuu Dar es Salaam kuwafutia mashtaka ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare na mwenzake Joseph Ludovick Rwezahura.
Hatua hiyo ya mahakama imefanya kiongozi huyo wa Chadema na mwenzake kuibwaga Serikali kwa mara ya pili mahakamani katika mashitaka dhidi yao.
Maombi hayo namba 5 ya mwaka 2014, yalifunguliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) katika Mahakama ya Rufani akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kufumfutia mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Uamuzi wa kutupilia mbali maombi hayo ulisomwa jana na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Zahra Maruma kwa niaba ya Jopo la Majaji watatu wa mahakama hiyo lililokuwa limepangwa kusikiliza maombi hayo.
Majaji hao ni Nathalia Kimaro (kiongozi wa jopo), William Mandia na Profesa Ibrahimu Juma.
Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa maombi hayo yalikuwa na dosari za kisheria kutokana na DPP kutoambatanisha mwenendo wa uamuzi wa Mahakama Kuu aliokuwa akiupinga.
Dosari hiyo iliibuliwa na Jaji Prosefa Juma katika tarehe ambayo maombi hayo yalikuwa yamepangwa kusikilizwa ambapo alihoji iwapo ni halali kusikiliza maombi hayo bila kuwepo kwa mwenendo huo.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Angaza Mwipopo akisaidiana na Wakili Serikali Mwandamizi, Hashim Ngole, alijibu kuwa wanachopinga ni uamuzi wa mahakama kufuta mashtaka katika kesi ambayo haikuwa mbele yake.
Wakili Angaza alidai kwamba kutokuwepo kwa mwenendo huo hakuathiri na kwamba mahakama ina uwezo wa kuyasikiliza maombi hayo hata bila kuwepo kwa mwenendo huo.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Lwakatare, Peter Kibatala alisema kuwa suala la mwenendo wa uamuzi unaopingwa ni miongoni mwa hoja za pingamizi lake la awali dhidi ya maombi hayo.
Wakili Kibatala alidai kuwa kutokuwepo kwa mwenendo huo ni dosari ambayo ina athari kubwa kiasi kwamba mahakama haitakuwa na uwezo wa kutoa kile kinachoombwa.
Alisisitiza kuwa kutokuwepo kwa kumbukumbu za mwenendo huo ni athari ambayo tiba yake ni mahakama kuyatupilia mbali maombi hayo.
Wakili Mwipopo alisisitiza kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 65 ya Kanuni za Mahakama ya Rufani, siyo lazima kuambatanisha mwenendo katika maombi na kwamba nyaraka za msingi kwa mujibu wa kanuni hiyo ni hati ya kiapo, ambavyo wameviambatanisha.
Hata hivyo, kupitia uamuzi wake jana, mahakama ilisema kuwa msimamo wa kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 4 (3) cha Sheria ya Mamlaka ya Mahakama ya Rufani ni lazima kuambatanisha mwenendo wa uamuzi unaopingwa, uamuzi na amri ya mahakama katika maombi ya marejeo.
“Kutokana na kasoro hiyo ya kutokuwepo kwa mwenendo wa uamuzi unaopingwa, tunatupilia mbali maombi haya,” ilisema mahakama katika uamuzi wake.
Katika maombi hayo, DPP alikuwa akiiomba Mahakama ya Rufani iitishe majalada ya kesi hiyo na kuchunguza uhalali wa uamuzi wa Mahakama Kuu kuwafutia washtakiwa hao mashtaka ya ugaidi na kisha ifute uamuzi huo wa Mahakama Kuu na amri zote ilizozitoa. Pamoja na mambo mengine, DPP alikuwa akidai kuwa haikuwa sahihi Mahakama Kuu kuamua kuwa mashtaka hayo hayakuwa halali, kwani hapakuwa na taarifa zilizowasilishwa dhidi ya washtakiwa, ambazo Mahakama Kuu ingezizingatia katika kuamua uhalali wake.
Kulingana na uamuzi huo, DPP anaweza kufungua tena maombi hayo baada ya kurekebisha kasoro hiyo, lakini baada ya kuomba kibali cha mahakama kufungua marejeo hayo nje ya muda wa kawaida kisheria.
Akizungumzia kesi hiyo, Lwakatare alisema: “Kwanza namshukuru sana Mungu kwa kuniwezesha kushinda kesi hii…; kusema kweli ilikuwa kesi ngumu na mbaya, hasa ikizingatiwa kwamba ilikuwa ndiyo kesi ya kwanza ya ugaidi kufunguliwa hapa nchini.”
Lwakatare aliongeza: “Nawashukuru mawakili wangu ambao wamekuwa wakisimamia kesi hii pamoja na makahama pia kwa kutenda haki leo (jana). Kama ungefanyika uamuzi tofauti na huu, basi ningebaki Segerea. Pia, haki hiyo imeweza kutendeka kutokana na misingi ya kesi husika kuwa ya kusuasua. Kesi ilifunguliwa kwa jabza na shinikizo la kisiasa.”
Alieleza kuwa, licha ya shinikizo hilo, haki imeweza kutawala na ameshinda kesi hiyo mbali na misukusuko aliyopitia.
Alisema kwamba anatumaini makahama itaendelea kutoa hati katika kutoa uamuzi wa kesi yake iliyobaki katika Makahama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Naye Wakili Kibatala alisema kuwa kwa hali ilivyo suala hilo limekwisha na kwamba DPP hana mwanya wa kurudi tena na maombi hayo.
Alifafanua kuwa kwa kawaida maombi ya marejeo hufunguliwa katika muda wa siku 60 tangu siku ya kutolewa kwa uamuzi unaopingwa na kwamba, nje ya muda huo mwombaji analazimika kuomba kibali cha Mahakama kufungua maombi nje ya muda na kutoa sababu za kuridhisha.
“Siku 60 tayari zimeshakwisha, hivyo DPP akitaka kurudi tena ni lazima aombe kibali na atoe sababu za kuiridhisha Mahakama. Sababu za kuridhisha ni pamoja na ugonjwa, au kuchelewa kupata nakala ya uamuzi na mwenendo kutoka mahakamani, lakini siyo kwa uzembe,” alisema.
Lwakatare na Ludovick walikuwa wakikabiliwa na mashtaka manne, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, matatu kati yake yakiwa ya ugaidi na moja la kawaida la jinai.
Mashtaka hayo ya ugaidi yalikuwa ni kupanga kumteka aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky na kisha kumdhuru kwa sumu, kushiriki mkutano wa vitendo vya ugaidi (kwa washtakiwa wote) na kuhamasisha vitendo vya ugaidi lililokuwa likimkabili Lwakatare pekee.
Shtaka lingine la jinai lilikuwa ni kula njama ya kutenda makosa, ambalo lilikuwa likiwakabili wote kwa pamoja na bado linaendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hata hivyo, Mei 8, mwaka huu Jaji Lawrence Kaduri wa Mahakama Kuu aliwafutia mashtaka ya ugaidi, baada ya mawakili wa Lwakatare kufungua maombi wakipinga uamuzi wa DPP kuwafutia mashtaka katika kesi ya awali na kisha kuwakamata na kuwafungulia mashtaka hayohayo.

No comments:

Post a Comment

 

Blogger news

Blogroll

LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZA KILA WAKATI

Receive all updates via Facebook. Just Click the Like Button Below

Powered By Blogger Widgets