Pages

Monday 1 September 2014

Kilichoinyima Siri ya Mtungi tuzo ya Afrika



NewsImages/7116250.jpg
wasanii wakijumuika katika picha
Thursday, April 17, 2014 6:59 PM
Siri ya Mtungi iliwania vipengele saba: Tuzo ya Mwigizaji Bora kwenye Drama, ikiwakilishwa na Juma Rajabu, Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Filamu za Vichekesho, Filamu Bora iliyotumia lugha kiufasaha (Kiswahili) na Mwandaaji Bora Mwenye Kipaji (Kyle Quint)
USIKU wa kuamkia March 9 Jumapili, haukuwa mzuri kwa tamthilia ya Siri ya Mtungi kwani ilichemka kwenye halfa ya tuzo za Africa Magic Viewers’ Choice Awards (AMVCA) 2014 zilizofanyika Nigeria.

Siri ya Mtungi tamthilia inayotengenezwa na Media for Development International (MFDI) Tanzania, ni tamthilia ilikuwa tishio kubwa katika tuzo hizo, kwani iliteuliwa kuwania vipengele saba tofauti kati ya vipengele 28 vilivyowaniwa.

Siri ya Mtungi iliwania vipengele saba: Tuzo ya Mwigizaji Bora kwenye Drama, ikiwakilishwa na Juma Rajabu, Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Filamu za Vichekesho, Filamu Bora iliyotumia lugha kiufasaha (Kiswahili) na Mwandaaji Bora Mwenye Kipaji (Kyle Quint).

Pia ilijitokeza kuwania Tuzo ya Mhariri Bora wa Sauti ikiwakilishwa na Jordan Riber, Tuzo ya Mbunifu Bora wa Mavazi (Doreen Estanzia Noni) na Tuzo ya Mpambaji Bora ikiwakilishwa na Rehema Samo.

Kwa bahati mbaya haikufurukuta hata kwenye kipengele kimoja, kutokana na kile kilichoelezwa na waandaaji kwamba Siri ya Mtungi ni kati ya washiriki waliopata kura chache katika kuwania tuzo hizo ambazo mshindi wake anategemea zaidi kura za watazamaji.

Tamthilia ya Siri ya Mtungi imeambulia patupu katika tuzo hizo zilizotolewa usiku wa kumkia jana Jumapili, katika Hoteli ya Eko and Suites Victoria Island, Lagos nchini Nigeria.

Akizungumza kwa njia ya barua pepe na gazeti hili jana, John Riber ambaye ni Prodyuza na Mkurugenzi Mkuu wa MFDI Tanzania, alisema: “Siri Ya Mtungi inawashukuru kwa kutuunga mkono, kwa nguvu kubwa na sasa tunajitayarisha kwa ajili ya tuzo nyingine mwakani. Tunatoa pongezi kwa wengine wote waliokuwa wamechaguliwa pamoja na washindi wote.”

Katika tuzo hizo ambazo hutolewa kila mwaka, Kenya imefanikiwa kutamba huku Nigeria ikiongoza kwa kutwaa tuzo nyingi zaidi. Waigizaji kutoka Nigeria waliotamba kwenye tuzo hizo ni pamoja na Osita Iheme, Rita Dominic na Desmond Eliot.

Vikwazo vilivyoiponza Siri ya Mtungi

Hakuna cha kuficha, Watanzania hatuna utamaduni wa kupiga kura. Tunaweza kuinuka na kusifia wenzetu pindi wanapofanikiwa, lakini kwa upande wetu hatuna utamaduni wa kuwafanya watu wetu wang’are.

Hata hivyo timu ya Siri ya Mtungi yenyewe haikuwa na nguvu kubwa kwenye kushawishi wadau, katika upigaji kura. Yote kwa yote timu hii ipo vizuri na tunaamini mapungufu haya yakirekebishwa, hakutakuwa na matatizo kama haya miaka ijayo.

Ni kweli kwamba penye ushindani daima kunakushinda na kushindwa, hivyo haina budi kukaza buti na kuanza kujipanga upya ili pindi tunapoanza tuwe washindi.
Hapana shaka wala wasiwasi, tuzo si kigezo pekee cha kupima ubora wa kazi. Hata wao wa mataifa mengine wamejifunza mengi, tayari elimu imewafikia ikiwa ndiyo lengo kuu la Siri ya Mtungi.

Watanzania wapo nyuma katika ushirikiano maana unakuta kazi nzuri na watu wanaikubali ila ikifika kwenye kupiga kura au kutoa maoni tunakuwa wazito.

Kiukweli tunapitwa na mambo mengi wakati tupo kwenye nafasi nzuri ya kushinda au kujitangaza. Siri ya Mtungi ni tamthilia nzuri kwa watazamaji wa kawaida na hata wale wageni wasioijua vyema lugha ya Kiswahili. Umoja ni nguvu daima.

Baadhi ya washindi wa AMVCAs kwa mwaka huu na kazi zao kwenye mabano ni pamoja na Shirley Frimpong (Manso), Yvonne Okoro & Ken Attoh (Contract), Frank Rajah Arase (The Groom’s Bride), Elvis Chucks ( A Wish), Bikiya Graham (Douglas) Flower Girl, Desmond Elliot ( Finding Mercy), Funke Akindele ( Return of Sheri Koko), Osita Iheme (The Hero), Walter Waltbanger Taylaur (The Wages), New Era Award Movie Rita Dominic (The Meeting) na wengineo.

Kuhusu Siri ya Mtungi

Ni tamthilia ya televisheni inayofurahisha, inayoonyesha maisha ya Cheche, mpigapicha mwenye bashasha na mmiliki wa studio ya kupiga picha ya Mtungi. Ana mke mrembo, Cheusi, aliyemzalia watoto wawili wenye afya huku akiwa na ujauzito wa mtoto wa tatu,’ hii ni sehemu ya kwanza ya tamthilia hiyo.

Ushiriki wa tamthilia hii katika tuzo hizi za kimataifa pia ni ishara ya kutambulika na kukua kwa sanaa na wasanii wa maigizo kutoka Tanzania. Sehemu ya pili ya tamthilia hii iliyojizolea umaarufu ndani na nje ya Tanzania ipo katika matengenezo na inatarajiwa kuanza kuonyeshwa tena ifikapo Mei mwaka huu.

John Riber Prodyuza na Mkurugenzi Mkuu wa MFDI Tanzania, anasema uamuzi wa kutayarisha tamthilia ya Siri ya Mtungi ya kiwango cha juu inayoongea moja kwa moja na watu wa Tanzania na Afrika Mashariki ni mwanzo wa kuleta mapinduzi ya mtandao wa mawasiliano.

Ndugu zangu tuchangie wasanii wetu.

No comments:

Post a Comment

 

Blogger news

Blogroll

LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZA KILA WAKATI

Receive all updates via Facebook. Just Click the Like Button Below

Powered By Blogger Widgets