UNAPOSOMA makala hii, huenda jua
limechomoza au huenda unajua litachomoza baada ya muda mfupi. Je, hilo
ni jambo muhimu? Naam, kwa sababu pasipo nuru ya jua, matrilioni ya
viumbe walio duniani—kutia na wewe—hawangekuwapo. Mamilioni ya viumbe
mbalimbali, kuanzia kwa bakteria wenye chembe moja hadi nyangumi wakubwa
mno wangeangamia wote.
Ni kweli kwamba ni takriban nusu
tu ya sehemu moja kwa bilioni ya nishati ya jua inayofikia sayari yetu.
Lakini, hata “kiasi hicho kidogo sana” cha “nuru” ya jua chatosha
kulisha na kutegemeza uhai duniani. Isitoshe, endapo kiasi hicho kidogo
sana cha nuru kinachotufikia kinaweza kutumiwa ifaavyo, kinaweza
kutosheleza mahitaji ya nishati ya jamii yetu ya kisasa kwa urahisi, na
bado kuwe na nishati ya ziada.
Vitabu vingi vya astronomia
vinasema kwamba jua letu ni nyota ya kawaida, “ni kitu cha kawaida tu
angani.” Lakini je, kweli jua ni “kitu cha kawaida tu angani”? Guillermo
Gonzalez, mwastronomia katika Chuo Kikuu cha Washington huko Seattle,
amedokeza kwamba jua letu ni la pekee. Je, hilo lapasa kuathiri jitihada
za kutafuta kuwapo kwa uhai katika sayari nyingine? Gonzalez ajibu:
“Tofauti na watu wanavyodhani, ni nyota chache sana zinazoweza
kutegemeza uhai wa viumbe wenye akili.” Aongezea hivi: “Waastronomia
wasipochunguza kwa makini sana nyota za pekee kama vile Jua, wanapoteza
wakati wao.”
Ni hali zipi zinazofanya jua letu
liweze kutegemeza uhai? Tunapochunguza hali hizo, tukumbuke kwamba
taarifa nyingi kuhusu fizikia ya ulimwengu ni za kinadharia.
Hali Zenye Kustaajabisha
● Nyota iliyo peke yake:
Waastronomia hukadiria kwamba asilimia 85 ya nyota katika ujirani wa
jua ziko katika makundi ya nyota mbili au zaidi, na kila nyota huzunguka
nyingine. Nyota hizo huunganishwa na nguvu za uvutano.
Hata hivyo, jua liko peke yake.
“Yaonekana hali ya jua kuwa peke yake ni jambo lisilo la kawaida,”
aandika mwastronomia Kenneth J. H. Phillips katika kitabu chake Guide to the Sun. Gonzalez asema kwamba hali ya jua kuwa peke yake huwezesha dunia izunguke kwa uthabiti zaidi, na hilo, hudumisha hali zinazositawisha uhai duniani.
● Nyota kubwa sana:
Hali nyingine ya pekee sana ya jua, kulingana na Gonzalez, ni kwamba
“liko miongoni mwa asilimia 10 ya nyota kubwa sana katika ujirani wake,”
laripoti gazeti la New Scientist. Phillips asema: “Jua
hufanyiza asilimia 99.87 ya mfumo wake. Nalo hudhibiti sayari nyingine
zote katika mfumo huo kwa nguvu zake za uvutano.”
Hali hiyo huiruhusu dunia kuwa
umbali wa kiasi kutoka kwa jua—kilometa milioni 150—na bado haiwezi
kuondoka mahali pake. Umbali huo mkubwa kwa wastani, hulinda viumbe
duniani wasiangamizwe na jua.
● Elementi nzito:
Gonzalez asema kwamba jua lina elementi nzito—kaboni, nitrojeni,
oksijeni, magnesi, silikoni, na chuma—zinazozidi kwa asilimia 50 zile
zilizo katika nyota nyingine yoyote iliyodumu kama jua na inayofanana
nalo. Jua letu halina kifani kwa habari hii. “Elementi nyingi nzito
zilizo juani si nyingi kupita kiasi,” asema Phillips, “lakini nyota
nyingine . . . zina elementi chache zaidi nzito.” Kwa hakika, nyota
zenye elementi nyingi nzito kama jua huwa katika kundi hususa la nyota
linaloitwa Population I.
Hilo lahusianaje na kuwapo kwa
uhai duniani? Kwa wazi, elementi nzito ni muhimu katika kutegemeza uhai.
Lakini ni adimu sana, ukubwa wake hauzidi asilimia 1 ya ulimwengu. Hata
hivyo, dunia yetu karibu yote hufanyizwa na elementi nzito. Kwa nini?
Kwa sababu waastronomia wanasema kwamba dunia huzunguka nyota ya msingi
isiyo ya kawaida—jua letu.
● Mzunguko ulio nusura duara: Kuna faida nyingine ya jua kuwa nyota aina ya Population I. “Kwa kawaida nyota za kundi la Population I huzunguka katikati ya galaksi kwa mzunguko ulio nusura duara,” chasema kitabu Guide to the Sun.
Mzunguko wa jua ni nusura duara tofauti na nyota nyingine zilizodumu
kama jua na zinazofanana nalo. Mbona hilo liathiri kuwapo kwa uhai
duniani? Kwa sababu umbo la duara la mzunguko wa jua huzuia jua
kutumbukia kwenye galaksi ya ndani, ambayo huwa na milipuko mingi ya
nyota (supernova).
● Kubadilika kwa mng’ao:
Hili ni jambo jingine lenye kupendeza kuhusu nyota ya mfumo wetu wa
jua. Mng’ao wa jua haubadiliki-badiliki kama mng’ao wa nyota nyingine
zinazofanana na jua. Yaani, jua hung’aa daima bila kubadilika-badilika.
Mng’ao huo madhubuti wa nuru ni
muhimu sana katika kutegemeza uhai duniani. “Kuwa kwetu duniani,” asema
mwanahistoria wa sayansi Karl Hufbauer, “huthibitisha kwamba mng’ao wa
jua ni mojawapo ya hali za mazingira zisizobadilika.”
● Mwinamo wa mzunguko:
Mzunguko wa jua umeinama kidogo tu kuelekea uso wa galaksi ya Kilimia.
Hilo lamaanisha kwamba pembe iliyopo kati ya uso wa mzunguko wa jua na
uso wa galaksi yetu ni ndogo sana. Hilo hutegemezaje masilahi ya viumbe
duniani?
Sehemu za mbali za mfumo wetu wa jua zimezingirwa na nyotamkia nyingi sana zenye umbo la tufe, ambazo huitwa wingu la Oort.*
Tuseme mwinamo wa mzunguko wa jua kuelekea uso wa galaksi yetu ungekuwa
mkubwa zaidi. Basi jua lingevuka uso wa galaksi yetu ghafula, na hivyo
kutibua wingu la Oort. Matokeo yangekuwa nini? Waastronomia wanasema
kwamba nyotamkia nyingi zingedondoka duniani na kusababisha maafa.
Kupatwa kwa Jua Kwafunua Nini?
Mfumo wetu wa jua una angalau
miezi 60. Miezi hiyo huzunguka sayari saba kati ya sayari tisa zilizo
kwenye mfumo huo. Hata hivyo, yaonekana dunia ndiyo sayari pekee ya mfumo wa jua ambamo kupatwa kwa jua kunakovutia hutukia. Kwa nini?
Jua hupatwa wakati mwezi
unapokuwa katikati ya jua na dunia. Ili mwezi ufunike jua kikamili, ni
lazima mwezi uwe karibu unalingana na jua. Na ndivyo inavyotukia!
Ijapokuwa kipenyo cha jua ni mara 400 zaidi ya kipenyo cha mwezi, umbali
kati ya jua na dunia ni mara 400 hivi ya umbali kati ya dunia na mwezi.
Lakini umbali wa dunia kutoka
kwa jua—na hivyo ukubwa wa jua—hauchangii tu kupatwa kwa jua. Ni muhimu
pia kwa uhai duniani. “Kama tungekuwa karibu zaidi au mbali zaidi na
Jua,” Gonzales asema, “Dunia ingekuwa moto sana au baridi sana kiasi cha
kutokalika.”
Kuna mengi zaidi. Mwezi ulio
mkubwa isivyo kawaida hutegemeza uhai kwenye sayari hii kwa sababu nguvu
zake za uvutano huzuia dunia kuyumbayumba sana kwenye mhimili wake.
Kuyumbayumba huko kungeweza kusababisha mabadiliko makubwa yaliyo hatari
ya hali ya hewa. Kwa hiyo ili uhai uwepo duniani, kinachohitajiwa ni
kipimo barabara cha umbali kati ya jua na dunia na vilevile mwezi wenye
ukubwa unaofaa—pamoja na hali nyinginezo zote zinazohusiana na hali ya
jua. Je, yawezekana kwamba yote hayo yalitokea kwa sadfa?
Je, Yalitokea kwa Sadfa?
Tuseme unapeleka gari lako kwa
fundi stadi aliyezoezwa ili alirekebishe. Ajitahidi kumaliza kazi hiyo,
nawe wapata gari likiwa sawa kabisa. Unafikiri atahisije iwapo
utasisitiza baadaye kwamba marekebisho sahihi ya gari lako yalitukia kwa
aksidenti tu au yalitukia kwa nasibu tu?
Twaweza kuuliza swali hilohilo
kuhusiana na hali ya pekee ya jua letu. Baadhi ya wanasayansi wanataka
uamini kwamba hali ya jua letu, mzunguko wake, na umbali wake kutoka kwa
dunia, na hali zake nyingine zote zilitukia kwa sadfa tu. Je, hilo
lasadikisha? Je, wafikiri ni mkataa wa kiakili?
Kama vile tu gari
lililorekebishwa kwa njia bora linavyodhihirisha uzoefu na ustadi wa
fundi, ndivyo na jua letu—na nyota nyingine za
kimbingu—linavyodhihirisha jambo fulani. Hali za pekee za nyota yetu ya
karibu inayotegemeza uhai duniani huwasilisha ujumbe dhahiri wa kwamba
nyota hiyo ni kazi ya mikono ya Mbuni na Muumba mwenye akili na nguvu
nyingi. Mtume Paulo alieleza hivi: “Sifa zake zisizoonekana zaonwa
waziwazi tangu uumbaji wa ulimwengu na kuendelea, kwa sababu zafahamiwa
kwa vitu vilivyofanywa, hata nguvu zake za milele na Uungu.”—Waroma 1:20.
No comments:
Post a Comment