Mnyama mkubwa anaibuka kutoka
baharini, ananyakua mashua nzima, na kuivuta pamoja na mabaharia chini
ya maji. Hadithi kama hizo zimesimuliwa kwa miaka mingi sana. Lakini je,
wanyama hao wakubwa ni halisi?
MNAMO 2007 ngisi anayeitwa colossal
alishikwa bila kukusudia na wavuvi katika Bahari ya Ross karibu na
Antaktika. Alikuwa na urefu wa mita 10 hivi, kutia na minyiri yake, na
alikuwa na uzito wa karibu kilogramu 500! Wanasayansi wanaamini kwamba
aina hiyo ya ngisi wanaweza kuwa wakubwa hata zaidi.
Mnyama mwingine mkubwa kama huyo anaitwa ngisi-jitu
ambaye ana mwili wenye umbo la kombora, macho yenye ukubwa wa kichwa
cha mwanadamu, mdomo kama wa kasuku wenye nguvu za kukata nyaya za
chuma, mikono minane yenye mashimo ya kufyonza, na minyiri miwili mirefu
ya kuvuta chakula hadi mdomoni. Akiwa majini anaweza kusonga kwa mwendo
wa kilomita 30 kwa saa, na hata anaweza kujirusha hewani!
Katika karne iliyopita inasemekana kwamba wanyama hao wakubwa walionekana mara zisizozidi 50, na hawajawahi kufanyiwa uchunguzi wakiwa baharini.
Nyangumi Wakubwa wa Baharini
Hata hivyo, ngisi-jitu na yule anayeitwa colossal ni chakula cha mnyama mwingine mkubwa zaidi, yule nyangumi anayeitwa sperm,
anayeweza kukua kufikia urefu wa mita 20 hivi na uzito wa tani 50. Jino
lake moja lina uzito wa gramu 900! Nyangumi wa aina hiyo wamepatikana
wakiwa wamekufa wakiwa na visehemu vya ngisi-jitu tumboni. Nyangumi hao
walikuwa na majeraha ya mviringo yaliyosababishwa na mashimo ya kufyonza
ya ngisi huyo, kuonyesha kwamba alipigana kwa ujasiri kabla ya kuliwa.
Mnamo 1965, kikundi cha wavuvi wa nyangumi kutoka Sovieti alidai kuwa
alijionea vita kati ya ngisi-jitu na nyangumi huyo mwenye uzito wa
tani 40. Hakuna aliyepona katika vita hivyo. Nyangumi aliyenyongwa
alipatikana akielea baharini akiwa na kichwa cha ngisi huyo tumboni
mwake.
Ingawa ngisi-jitu na nyangumi huyo anayeitwa sperm ni wakubwa sana, nyangumi wa rangi ya bluu-kijivu,
ambaye ndiye mnyama mkubwa zaidi kati ya wanyama wanaonyonyesha,
anawazidi kwa ukubwa. Nyangumi wa kike wa aina hiyo mwenye urefu wa
mita 33 aliyevuliwa huko Antaktika ndiye nyangumi mrefu zaidi kuwahi
kurekodiwa. Nyangumi wa rangi ya bluu-kijivu anaweza kuwa na uzito wa
tani 150 hivi. Uzito wa ulimi wake peke yake ni sawa na uzito wa tembo
aliyekomaa! Hebu wazia—nyangumi huyo huzaa mtoto mwenye uzito wa tani
tatu na urefu wa mita 7 hadi 8! Kwa sababu ya kuvuliwa sana na wavuvi wa
nyangumi, nyangumi huyo karibu atoweke katika miaka ya 1960 na leo
amewekwa katika orodha ya wanyama walio katika hatari kubwa ya kutoweka.
Wanyama Wakali na Wapole
Kwa sababu ya meno yake 3,000, huenda papa mweupe
akawa ndiye samaki mla nyama mwenye kutisha zaidi. Papa mweupe mkubwa
zaidi kuwahi kurekodiwa alikuwa na urefu wa mita 7 na uzito wa kilogramu
3,200. Papa huyo ana uwezo mkubwa ajabu wa kunusa, kwani anaweza kunusa
tone moja tu la damu linapochanganywa katika maji ya lita 100!
Samaki mkubwa zaidi ni papa nyangumi
mwenye urefu wa mita 7.5 hivi. Hata hivyo, wengine wanaweza kuwa na
urefu mara mbili ya huo. Mdomo wake unaweza kupanuka kwa mita 1.4 na
hivyo anaweza kummeza mwanadamu kwa urahisi. Lakini badala ya kuwa
mwindaji hatari wa wanyama wengine wakubwa wa baharini, samaki huyu
mkubwa hula mimea ya baharini na samaki wadogo.
Likizungumza kuhusu simulizi la Biblia la nabii Yona aliyemezwa na samaki mkubwa, gazeti National Geographic lilisema kwamba “umeng’enyaji wa ajabu
wa papa nyangumi hufanya tuamini hadithi kama ile ya Yona.” Papa
nyangumi “huondoa tumboni kwa njia isiyodhuru vitu vikubwa wanavyomeza
ambavyo haviwezi kumeng’enywa.”—Yona 1:17; 2:10.
Jitu Linalopenda Kujificha
Kiumbe mwingine mkubwa wa baharini ni pweza mkubwa,
ambaye anaweza kukua na kufikia uzito wa kilogramu 250 hivi. Wakati
mmoja aliitwa samaki-ibilisi, kwa kuwa ilidhaniwa anaweza kuzamisha
meli. Hata hivyo, pweza huyo hujificha sana kwenye sakafu ya bahari
katika mashimo na nyufa. Mikono yake minane ina urefu wa mita 10 hivi,
na pweza ndiye mnyama aliye na ubongo mkubwa zaidi kati ya wanyama wote
wasio na uti wa mgongo. Kwa kweli, pweza wana akili nyingi sana na
wanaweza kujifunza kufanya mambo ya ajabu kama vile kufumbua mafumbo na
kufungua vifuniko vya chupa!
Kama tu ngisi-jitu, pweza mkubwa
anaweza kujificha kwa kubadili rangi, anaweza kujirusha juu kwa nguvu,
na anaweza kuepuka hatari kwa kutoa wingu kubwa la rangi. Pweza anaweza
hata kutoka majini kwa muda mfupi ili atafute chakula kwenye nchi kavu!
Viumbe hao wa baharini hulisifu
sana jina la Muumba wao, Yehova. Ndiyo sababu mtunga-zaburi wa Biblia
aliimba hivi: “Msifuni Yehova kutoka duniani, enyi wanyama wakubwa wa
baharini, nanyi vilindi vyote vya maji.”—Zaburi 148:7.
No comments:
Post a Comment