Pages

Wednesday 8 April 2015

RAIS JK AANIKA MAGUMU KATIKA UTAWALA WAKE!




Dar es Salaam. Wakati makada wa CCM wakipigana vikumbo kuwania kupitishwa na chama chao kuwania urais, Rais Jakaya Kikwete anayemaliza ngwe yake amesema nafasi hiyo ni kadhia, ni kazi ngumu na si ya kukimbilia.

Rais Kikwete aliyasema hayo juzi nchini Marekani, wakati akihutubia kwenye taasisi inayoitwa, Woodrow Wilson International Center for Scholars, ambapo alitumia muda huo kuelezea mafanikio na changamoto katika kipindi chake cha miaka 10 ya uongozi wake.

“Wakati unaingia Ikulu unakuwa na shauku kubwa sana pamoja na furaha ya ushindi, lakini kwa hakika urais ni kadhia kubwa, ukipata fursa ya kuwa rais kwa awamu mbili kama mimi, nadhani zinatosha kabisa, nimefanya mengi kwa nchi yangu, atakayekuja ataendeleza nilipoishia,” alisema Rais Kikwete.

Alitumia fursa hiyo kuieleza dunia kwamba baada ya kustaafu nafasi yake Oktoba baada ya Uchaguzi Mkuu, atatumia muda wake mwingi kujihusisha na kilimo, lakini anajipanga pia kuanzisha taasisi itakayojishughulisha na masuala ya vifo vinavyotokana na uzazi pamoja na malaria.

Alisema akitazama nyuma mwaka 2005 alipokuwa anaingia Ikulu, hana cha kujutia mpaka sasa anapojiandaa kuondoka Ikulu ya Magogoni, ila anasema amejifunza mambo mengi.

“Ninaamini kwamba mrithi wangu ataendeleza pale nilipoishia, ninachoweza kujivunia ni kwamba tumeweza kujenga misingi imara katika kulielekeza Taifa letu kwenye Dira ya Maendeleo 2025, ambayo imejikita katika kuifanya nchi yetu kuwa ya uchumi wa kati,” alisema Rais Kikwete.

Aliongeza, “Ninadhani nitaweza kuacha sera madhubuti ya masuala ya uchumi wa gesi pamoja na mapato ambayo matunda yake yataanza kuonekana 2020. Bila shaka tutakuwa na uchaguzi huru, haki na kwamba ninaisubiri kwa hamu siku ya kuikabidhi Ikulu kwa rais ajaye,”


Utengamano wa kitaifa 
Akijibu swali la mwongoza mjadala, Monde Muyangwa kuhusu ni namna gani amefanikisha kuliweka Taifa pamoja mbali na changamoto zilizopo duniani kote, Rais Kikwete alisema ni kutokana na misingi ambayo imeachwa na waasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Karume.

“Katika kipindi changu kumekuwa na changamoto za kutaka kutumia madhehebu ya dini kisiasa, nimekuwa mstari wa mbele kukemea matukio hayo.

“Nimekuwa natumia muda wangu kukutana na viongozi wa dini kuwakumbusha umuhimu wa amani tuliyonayo pamoja na dhamana wanayobeba katika jamii,” alisema Kikwete. Alisema Tanzania ni nchi ambayo ina makabila takriban 120, pamoja na rangi mbalimbali na Watanzania wengi ni wafuasi wa dini na baadhi wakiwa hawana dini na pengine bado hawajaamua kuchagua, lakini wote wanaishi pamoja.

Alisema baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, kulianza kuwa na dalili za kutofautiana kimtazamo kitu ambacho kingeweza kutarisha Amani na mshikamano wa Taifa.
 

Vurugu za kisiasa Zanzibar 
Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM alisema, haikuwa kazi rahisi kuleta uwiano wa kisiasa hasa Zanzibar, ambako kumekuwa na mzozo wa kiasiasa baina ya vyama vikubwa viwili vya CCM na CUF. 

“Mvutano huo ulikuwa mkubwa sana kiasi cha kutishia mgawanyiko baina ya visiwa hivyo. Ninajivunia kwamba nimeendelea kuilinda nchi yangu kama walivyofanya watangulizi wangu. Nimekuwa nikizitatua changamoto zinazotishia umoja wetu,” alisema.

Aliongeza kuwa, “Mwafaka wa kisiasa uliopatikana baina ya vyama viwili vya CCM na CUF huko Zanzibar, umekuwa kichocheo kikubwa kwa uchaguzi wa kistaraabu visiwani humo.”

No comments:

Post a Comment

 

Blogger news

Blogroll

LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZA KILA WAKATI

Receive all updates via Facebook. Just Click the Like Button Below

Powered By Blogger Widgets