Pages

Saturday, 9 May 2015

MATUKIO YA ANGANI KWA MWAKA 2013


Miongoni mwa matukio makubwa yanayotegemewa mwaka huu ni kupatwa kwa Jua na kupatwa kwa Mwezi, pamoja na uwezekano wa kuonekana kwa kimondo kikubwa.  Mwaka huu, sayari mbali mbali zilizo jirani yetu zitaendelea kujitokeza katika anga nyakati za usiku hapa Tanzania.  Pamoja na yote, anga letu la kujivunia litaendelea kun’gaa kwa nyota za kusisimua.
Tukio linalo subiriwa kwa hamu kubwa   ni lile la kupatwa kamili kwa Jua siku ya Jumapili, tarehe 3 Novemba 2013, litakalotokea jirani na nchi yetu.  Kivuli cha Mwezi kitatua Duniani kuanzia Bahari ya Atlantiki na kuingia Afrika pale Gabon.  Baada ya hapo kivuli kitapita kaskazini mwa Uganda na Kenya saa za jioni na kuishia kusini mwa Ethiopia wakati wa magharibi. Mahali muafaka zaidi pakuangalia Jua likizibwa kabisa na kusababisha giza kabisa ni kaskazini mwa Kenya, karibu na Ziwa Turkana, ambako kupatwa kamili kutatokea saa 11:25 jioni kwa muda wa sekunde 14 tu.  Hapa Tanzania tupo kusini kidogo tu ya sehemu ambako Jua litapatwa kamilifu.  Kwa hiyo siku hiyo ya Novemba 3, sisi tutashudia kupatwa kwa sehemu ya Jua hadi kufikia asilimia 70%. 
Mwaka huu, Jua litapatwa pia tarehe 10 Mei, lakini hatutaona nchini Tanzania kwa vile tukio litatokea upande wa pili wa Dunia katika Bahari ya Pasifiki.

Mwezi utapatwa mara tatu mwaka huu,  na mara zote kivuli chepesi tu kitatanda juu ya sura ya Mwezi.  Hata hivyo, tukio la tarehe 25 Aprili 2013, litakalotokea juu ya anga za Afrika na Bahari ya Hindi, kwa hiyo kivuli, ingawa ni chepesi, kitakolea zaidi hapa kwetu kwa vile Mwezi wote utazama ndani ya kivuli hicho chepesi.  Mn’garo wa sura ya Mwezi ambayo itakuwa katika hali ya upevu siku hiyo, inategemewa kufifia kiasi cha kutosha kwa sisi kuweza kutambua kupungua kwa ung’avu wa sura ya Mwezi.  Kwa hiyo itavutia sana kuona namna mwanga mkali wa mwezi mpevu unavyopunguzwa na kivuli hafifu.  Pamoja na hiyo, sehemu ndogo ya ukingo wa Mwezi, upande wa kaskazini, itafunikwa na kivuli kizito kwa hiyo ni changamoto ya kutosha kuweza kutambua chembe ya ukingo wa kushoto ikiwa imezibwa na kivuli kizito.
Mwezi utapatwa tena siku ya tarehe 25 Mei  na tarehe 19 Oktoba 2013.  Katika tukio la 25 Mei, sehemu ndogo tu ya Mwezi itaingia ndani ya kivuli chepesi, kwa hiyo macho yetu hayataweza kutambua kuwa Mwezi umepatwa.  Siku ya tarehe 19 Oktoba, zaidi ya theluthi mbili ya mwezi itaingia ndani ya kivuli chepesi.   Watazamaji makini wanaweza wakatambua tofauti kati ya ung’avu wa Mwezi mpevu kabla ya kupatwa, na ule wa baada ya kupatwa.
Tukio lingine linalosubiriwa kwa shauku kubwa ni la kujitokeza kwa kimondo kikubwa ambacho kinategemewa kung’ara
zaidi kuliko vyote.
  Kimondo hicho kinategemewa kujitokeza katika anga zetu mwishoni wa mwaka huu. Kimondo ISON, kimegunduliwa mwaka jana tu, mwezi Septemba,  kikiwa umbali mkubwa wa kilometa bilioni mbili kutoka Duniani.   Jinsi kimondo kinavyozidi kutukaribia, nacho kinazidi kujidhihirisha.  Tarehe 28 novemba kimondo kitakuwa umbali wa kilomita milioni mbili kutoka kwenye Jua na tena ndani ya anga za Jua.  Iwapo kimondo ISON hakitavunjwa na nguvu ya mvuto wa Jua, ambayo inaweza ikaipa kimondo kasi kali ya kilometa laki tano kwa saa, tutaweza kufaidi kuona kimondo kikubwa kuliko vyote vilivyowahi kuonekana na hata kuwaka wakati wa mchana.  La sivyo tutapata dalili tu za vipande vipande vya kimondo hicho.
Barafu inayounda kimondo huvukiza (muyeyuko wa kufanya mvuke) kimondo kinapopashwa moto na joto la Jua.  Upepo wa Jua hupeperusha vumbi laini kwenye kimondo, na kusukuma vumbi hiyo umbali wa mamilioni ya kilomita nyuma ya kimondo. 
Hali hii hukipa kimondo umbo la mkia mrefu. Kimondo hicho kwa sasa kinafuatiliwa kwa makini sana na Wanaastronomia duniani kote kuangalia jinsi kinavyozidi kubadilika kadri kinavyokaribia duniani.
Miongoni mwa sayari angani, Jupita (Mshatrii au Sambulaa) inaanza mwaka ikiwa angavu kwenye mbingu za usawa wa utosi, na itabaki angavu na kuonekana hadi Juni.  Kwa sasa Zohali (Saturn) ni nyota ya alfajiri inayoangaza upande wa magharibi. Inaingia katika mbingu za jioni katikati ya mwezi Aprili kwa kuchomoza upande wa mashariki mapema jioni.  Itasogea magharibi pole pole na hadi mwanzo wa Oktoba itakuwa katika anga za magharibi saa za jioni.  Baada ya hapo itatoweka angani. Zohali huonekana mbinguni kama nyota angavu inayobainika zaidi miongoni mwa nyota nyingine kwa sababu haimetimeti. Mars (Meriki) nayo huanza mwaka kwa kuonekana kama nyota nyekundu hafifu hadi Machi wakati inapotoweka mbinguni.
Zuhura (Venus) ni nyota ya alfajiri mwanzoni mwa mwaka ikiwa mwinuko wa nyuzi 20 juu ya upeo wakati wa mapambazuko.  Itateremka hadi itakapokuwa karibu zaidi na Jua na kutoonekana baada ya mwisho wa Februari na kuanza kuonekana tena mwanzoni mwa Mei na kuanza kung’ara tena kama nyota ya jioni. Ifikapo tarehe 26 Mei, Zuhura, Jupita na Zebaki zitaunda pembetatu ya kupendeza angani, na zitakuwa karibu kabisa tarehe 28 Mei.  Sayari tatu hizo zitajipanga angani kwa mstari ulioonyoka tarehe 31 Mei 2013.
Zebaki itan’gara kupita kiasi wakati itakapojitokeza mwezi Mei na itabainika karibu na jozi iliyoangavu zaidi ya Zuhura na Jupita. Zebaki ni sayari inayozunguka karibu sana na Jua, kwa hiyo kuonekana kwake kutokuwa juu zaidi mbinguni. Hata hivyo mwaka huu itaonekana mara tatu juu kwa mwinuko wa nyuzi 20 juu ya upeo, wakati wa Jua kuchwa.  Mwanzoni mwa Mei hadi katikati ya Juni Zebaki itainuka hadi nyuzi 20 tarehe 23 mei.  Kuanzia katikati ya Agosti hadi mwanzoni mwa Oktoba na kuwa na mwinuko wa juu zaidi wa nyuzi 22, tarehe 19 Septemba 2013.
Kila siku Mwezi hubadilisha nafasi yake angani kwa kusogea kiasi cha nyuzi 12, kwa hiyo mara kwa mara huchukua nafasi za kuvutia angani karibu na nyota na sayari angavu.  Mwezi utakuwa karibu zaidi na jozi ya Zuhura na Zebaki tarehe 10 Juni, na hivyo utaunda mstari na jozi hiyo na kutoa mwonekano wa kuvutia kwenye mbingu za upeo wa magharibi kiasi cha nyuzi 20 juu ya upeo baada tu ya Jua kuchwa.
Miunganiko mingine ya karibu ya kuvutia ni tarehe 14 Aprili wakati itaunda mstari na Jupita na nyota kubwa nyekundu ya Aldebaran katika anga la utosini. Tarehe 8 Septemba Mwezi utakuwa karibu sana na Spika ambayo ni nyota angavu zaidi katika kundi la nyota la Mashuke, na Zuhura itakuwa karibu upande wa pili.
Kati ya Septemba 6 na 10, Zebaki, Zuhura, Zohari naMwezi zitaunda mstari angani, huku Mwezi ukibadili nafasi yake siku hadi siku ndani ya mstari huo. Mstari kama huu hujulikana kama njia ya Jua, kwa vile sayari zote pamoja na Mwezi na Jua huonekana katika mstari huu tu. Hii ni kwa vile sayari zote katika mfumo wa Jua huzunguka Jua katika bapa moja.  Kwa muono wetu wa anga kutoka Duniani, bapa hiyo inakuwa ni mstari angani.  Tarehe 6 na 7 Oktoba, Mwezi utaunda pembe tatu na Zebaki na Zohali.
Taarifa za karibu zaidi zitatolewa kadri mwaka unavyoendelea au angalia tovuti hii, http://www.astronomyintanzania.or.tz ili uweze kuandaa mapema mpango wako wa vipindi vya kuangalia nyota.
Kampeni ya Dunia Wakati wa Usiku (Globe at Night), ambayo ni jitihada ya kufuatilia uchambuzi wa uagavu wa anga za usiku hufanywa na watu wa kawaida Duniani kote wanaopenda kuangalia anga pamoja nyota na sayari.  Kampeni hiyo hutumia muono wa nyota angavu zinazoonekana katika vipindi mbali mbali vya mwaka.  Watazamaji wanabainisha hali ya uchafuzi wa mazingira kwa mwanga na kutoa taarifa kwenye tovuti kuu ya kampeni hiyo kuhusu jinsi wanavyoziona nyota hizo angavu kwenye maeneo yao. Mwaka huu kampeni inaendeshwa Januari 3-12, Januari 31 hadi Februari 9, Machi 3-12, Machi 31 hadi Aprili 9, na Aprili 29 hadi Mei 8.  Hii ni nafasi yako ya kushiriki katika uchunguzi wa kisayansi ya ulimwengu wetu.  Angalia tovuti http://www.globenight.org kwa maelezo ya namna ya kushiriki na kupeleka matokeo ya muonekano wa nyota sehemu unakoishi. 

No comments:

Post a Comment

 

Blogger news

Blogroll

LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZA KILA WAKATI

Receive all updates via Facebook. Just Click the Like Button Below

Powered By Blogger Widgets