Kikundi cha wanajiolojia watafiti

Katika makala haya, tutaangalia jinsi wanasayansi wa kawaida, tena ambao walikuwa hawaamini  kabisa kwamba kuna Mungu au shetani, katika utafiti wao ambao haukuwa na uhusiano wowote na masuala ya rohoni, walijikuta wanagundua mambo ambayo yaliwatia hofu hadi wengine kukimbia kazi. Waliweza kusikia waziwazi sauti za vilio vya mateso kutokea katikati ya dunia! Sauti hizo walizirekodi; na mwisho wa makala haya utaona anwani inayoweza kukupeleka kuzisikia sauti hizo za kutisha na kusikitisha mno, mno!!

Ni nani ambaye hajasikia habari za kwamba wanga huenda baharini, wakatupa mayai viza kisha malango yanafunguka nao wanashuka hadi kuzimu? Bila shaka habari hizi si ngeni masikioni mwa wengi wetu? Ni mambo ambayo ni rahisi kuaminika katika ulimwengu wa kawaida lakini unapoyaongelea kwa mtazamo wa Biblia, hapo watu wanaanza kukosa imani na kudhani kuwa si za kweli.

Makala haya yanatokana na habari ambayo iliandikwa katika gazeti la Ammennusatia la kule Finland katika toleo lake la Julai 1989.

       Sehemu ya gazeti

Kikundi kimoja cha wanajiologia (wana elimu ya miamba) wa Kirusi walikuwa katika mradi wa kutoboa tundu katika eneo la Kola, karibu na Murmansk; maili takriban 150 kaskazini mwa Duara la Aktiki, nchini Siberia. Watafiti hao waliweza kutoboa tundu ardhini lenye urefu wa kilometa 14.4 kwenda chini.

Dr Azzacov, ambaye alikuwa ndiye meneja wa mradi alisema kuwa wakati wa kutoboa, ghafla drili ilianza kuzunguka bila utaratibu, hali iliyoonyesha kwamba drili imefika kwenye sehemu iliyo na uwazi.

“Taarifa tunazokusanya ni za kushangaa sana, kiasi kwamba kwa kweli tumeingiwa na hofu maana hatujui kile tunachoweza kukikuta huko chini,” alisema Dr Azzacov. 

“Jambo la pili lililotushangaza lilikuwa ni kiwango cha joto tulichokigundua katikati ya dunia. Mahesabu yanaonyesha kuwa joto hilo lilikuwa takribani nyuzi 1,000 za Selsiasi,” aliongeza kusema Dr Azzacov. “Hii ni zaidi ya kile tulichotegemea. Inaonekana ni kama moto wa jehanamu unawaka kwa nguvu sana humo ndani, katikati ya dunia!”

“Ugunduzi wa mwisho ndio uliokuwa wa kushitua sana masikioni mwetu kiasi kwamba wanasayansi wana hofu kubwa ya kuendelea na mradi huu. Tulikuwa tukijaribu kusikiliza mjongeo wa dunia kila baada ya muda fulani kwa kutumia vinasasauti vya hali ya juu sana (supersensitive microphones), ambavyo tulikuwa tukivishusha hadi chini kupitia kwenye tundu tulilotoboa.”                                                                                 

Dr Azaccov anaendelea kueleza kwamba, “Kile tulichosikia, wanasayansi hawa ambao wamezoea tu kuamini mambo yanayoleta mantiki akilini, kiliwafanya kutetemeka kwa hofu kubwa mno!  Wakati mwingine hicho tulichokisikia kilisikika kwa sauti ya chini lakini kali ambayo mwanzoni tulidhani inatokana na vifaa vyetu.”                                                                                                                 

“Lakini baada ya kuvirekebisha, tulibaini kwamba zilikuwa ni sauti zilizotoka katikati ya dunia kabisa. Hatukuamini masikio yetu. Tulisikia sauti ya mwanadamu akipiga kelele kwa maumivu. Japokuwa sauti moja ilikuwa inasikika kwa uwazi zaidi, tuliweza kusikia kwa nyuma sauti za maelfu, na huenda mamilioni ya watu wakilia kwa mateso na maumivu.

“Baada ya ugunduzi huu wa kutisha, nusu ya wanasayansi waliachana na mradi huo kutokana na hofu. Ni matumaini yangu kuwa hicho kilichoko huko chini kitabia hukohuko,” aliongezea Dr Azzacov.

“Na kilichowamaliza kabisa nguvu hawa wanasayansi wa Kisovieti, mbali na hizo sauti walizozisikia, ilikuwa ni kutokea usiku uleule kwa gesi inayong’aa kutoka kwenye tundu lile walilokuwa wamelitoboa; na katikati yake alijitokeza kiumbe mwenye mabawa kama ya popo pamoja na maneno yaliyokuwa yameandikwa kwa Kirusi ‘Nimeshinda’.”

Baada ya mkasa huo, Dr Azzacove alisema, “Mimi kama mkomunisti, siamini juu ya mbingu au Biblia, lakini kama mwanasayansi, hivi sasa naamini juu ya kuwapo kwa kuzimu. Ni kweli tuliogopa sana kutokana na ugunduzi huo. Lakini tunajua fika kile tulichokiona na kukisikia. Tunaamini kabisa kuwa tulitoboa tundu kwenye lango la kuzimu yenyewe!”

MAELEZO YANGU MIMI JIMMY

Hili lilikuwa ni tukio ambalo liliwatokea watu ambao hawaamini kabisa habari ya Mungu. Wengi tunakumbuka kwamba kabla ya kusambaratika kwa Urusi ya zamani, ambayo ilikuwa ni dola kubwa ya umoja wa nchi za kisovieti, itikadi ya kisiasa ya dola hiyo ilikuwa ni ya kikomunisti ikiongozwa na falsafa za akina Marx, Lennin, Angels na Stalin.

Wao waliamini katika uyakinifu (materialism), yaani kwamba mwanadamu pamoja na ulimwengu wote ni kile tu kinachoonekana kwa macho au kuthibitika kisayansi. Suala la Mungu, shetani na chochote cha kiroho kwao kilikuwa ni uzushi. Na yeyote aliyejaribu kueneza itikadi za kidini, alishughulikiwa na dola ipasavya.

Karl Marx, kwa mfano , alisema, “Religion is an opium dose of the people.” – kwamba, “Dini ni dozi ya afyuni (dawa za kulevya) kwa watu.” Hii ikimaanisha kwamba dini ni kama ulevi wa kupumbaza akili za watu na kuwafanya wasiendelee.

Kwa hiyo, haingewekana kabisa wakomunisti hawa waanze kueleza mambo ya rohoni ambayo maishani mwao mwote, tangu wakiwa watoto, waliaminishwa kwamba hakuna Mungu wala shetani, kama anavyokiri Dr Azzacov mwenyewe kwenye maneno yake ya mwisho.

Sasa je, ugunduzi wao huo uliowajia bila kutegemea una uhusiano wowote na Biblia?

Biblia inasema kwamba Yesu amepewa heshima kubwa na Mungu: “… ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi.” (Wafilipi 2:10). Chini ya nchi hapa ni kuzimu!

Katika kuongelea kuhusu kupaa kwa Bwana Yesu, maandiko yanasema: “Basi neno hilo, Alipaa, maana yake nini kama siyo kusema kwamba yeye naye alishuka mpaka pande zilizo chini za nchi?” (Waefeso 4:10). Pande zilizo chini za nchi hapa ni kuzimu!

Je, Yesu alienda kufanya nini huko?

Biblia inasema kwamba Yesu alipoteswa: “… mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa, ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiri.” (1 Petro 3:18-19). Yesu hakuhubiri tu duniani, bali kwa zile siku tatu alizokaa kaburini, alienda kuwahubiria wale wote waliokuwa wamekufa tangu Adamu hadi wakati huo Yeye alipokufa.Kifungoni hapa ni kuzimu!

Maandiko haya matatu (japo yapo na mengine), yanatuonyesha kwamba ni kweli chini ya dunia ndiko iliko sehemu inayoitwa kuzimu; ambayo ndiyo makao ya shetani na mapepo au majini; ambako watu wanaokufa katika dhambi wanaenda kuanza mateso wakisubiri siku ya mwisho wa ulimwengu.

HITIMISHO

Licha ya kwamba kuzimu kuna mateso makali yasiyoelezeka, lakini ukae ukijua kwamba kuzimu si jehanamu! Kuzimu ni makao ya shetani na majini wake leo; lakini jehanamu ni moto ambako mashetani au majini pamoja na watenda dhambi wote watatupwa na Bwana Yesu baada ya mwisho kabisa wa ulimwengu.

Biblia inasema hivi: Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti. (Ufunuo 20:10).

Pia imeandikwa: Mauti na kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani hilo ziwa la moto. Na iwapo mtu yeyote hakuonekana ameandikwa kwenye kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto. (Ufunuo 20:14-15).

Sasa, kama kuzimu tu kuna mateso yasiyoelezeka, je jehanamu itakuwa vipi?

Biblia inasema: Ni jambo la kutisha kuanguka katika mikono ya Mungu aliye hai. (Waebrania 10:31). Hii ni kwa sababu wanaoangukia mikononi mwa shetani wanaweza kupata fursa ya kuokolewa; lakini ukiangukia kwa Mungu mwenyewe, ni nani tena wa kukuokoa??

Ndugu unayesoma makala haya, pokea wokovu wa Bwana Yesu muda ungalipo, maana Biblia inasema “Wakati uliokubalika ni sasa” (si leo)! Nimeshasema mara kadhaa, dini haina wokovu; NI YESU PEKE YAKE ANAYEOKOA! Dini bila Wokovu wa Yesu ni maagizo tu ya wanadamu.

Habari za Dr Azzaccov na timu yake unaweza kuzisoma mwenye mtandaoni kwenyewww.diggsjourney.com. Hata hizo sauti za watu wanaoteseka kuzimu ambazo walizirekodi zimo humohumo; ni vizuri uzisikilize!!

Karibu kwenye makala nyingine kama Bwana Yesu atakuwa bado hajarudi.