WATU wengi wanadhani kuwa utafiti kuhusiana na wanyama umekamilika.
Lakini ukweli ni kuwa bado kuna maswali mengi sana kuhusiana na maisha
ya wanyama mbalimbali ambayo hayajapatiwa majibu.
Ndio maana kila kukicha unajitokeza ugunduzi mwingine mpya ambao mara
nyingi unawaacha watafiti vinywa wazi lakini baadaye unatoa mwanga wa
masuala kadhaa waliyokuwa hawayaelewi awali.
Mathalani, tunafahamu visa kadhaa vya watoto kuzaliwa wakiwa wameungana.
Lakini hivi karibuni watafiti wa huko Mexico walimgundua nyangumi wa
kijivu walioungana.
Inaaminika kuwa hili ni tukio la kwanza duniani la kupatikana kwa nyangumi pacha wa aina hii walioungana.
Zipo taarifa nyingine za nyangumi walioungana lakini taarifa hizo
hazijafanywa kuwa rasmi. Ndio maana watu wengi, wakiwamo watafiti
wanaamini kuwa hili litakuwa tukio la kwanza na la kuweka rekodi
kuhusiana na nyangumi pacha wa kijivu waliungana.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya sana, pacha hao waligunduliwa wakiwa tayari
wameshafariki. Inaaminika kuwa walifariki hata kabla hawajazaliwa.
Inaaminika kuwa ilikuwa ni mimba iliyoharibika kwa sababu mzoga huo
ulikuwa na urefu wa futi saba wakati nyangumi anazaliwa akiwa na urefu
wa futi kati ya 12 na 16.
Mtafiti mmoja kutoka Marekani Alisa Schulman Janiger, anasema uchunguzi
wake ulibaini kuwa pacha hao walikuwa hawajafikia hatua ya kuzaliwa.
Lakini pia anaamini kuwa kuna uwezekano wa watoto hao kuuawa na mama
yao.
Pamoja na kuwa pacha hao wa nyangumi walioungana waligunduliwa wakiwa
wameshakufa, lakini mabaki yake yalikusanywa na kuhifadhiwa kwa ajili ya
utafiti wa kina.
Ni kawaida kwa nyangumi wa kijivu kufika katika eneo hilo la Scammon na
maeneo mengine yanayofanana na hilo katika ufukwe wa Baja huko
California, baada ya safari ya karibu kilometa 6,000 kutoka maeneo ya
Arctic ambako huishi kwa kipindi kirefu.
Katika safari hii kuelekea maeneo ya kusini ndipo wanapozaa katika
maeneo hayo ya lagoon na kuwatunza watoto wao kwa wiki kadhaa kabla
hawajaanza safari ya kurejea kaskazini ambako ndiko kwenye makazi yao
katika bahari za Bering na Chukchi.
Watoto wengi huzaliwa katika wiki ya mwisho ya Disemba na wiki mbili za
kwanza za Januari kila mwaka. Kwa mujibu wa taasisi ya NOAA, idadi ya
nyangumi wa kijivu katika bahari ya Pacific ni kama 21,000.
Ukiachana na nyangumi hawa walioungana ambao wameleta mwanga mpya katika
sayansi ya viumbe wa baharini, pia kuna tukio jingine la kuvuliwa kwa
kiumbe mwingine mkubwa katika eneo la bahari ya Florida.
Kutokana na ukubwa wake ilikuwa ni vigumu kufahamu hasa yeye ni samaki
wa aina gani ingawa utafiti wa awali unaonesha kuwa anaweza kuwa papa.
Alivuliwa na mvuvi Mark Quartiano ambaye amebatizwa jina la mvua papa
kutokana na umahiri wake wa kuvua samaki aina ya papa. Mark tayari
ameshakamata maelfu ya samaki hao, lakini hii ilikuwa ni mara yake ya
kwanza kumvua kiumbe wa ajabu kama huyo aliyekuwa na uzito wa paundi 800
katika maeneo ya fukwe za Miami.
Mark mwenyewe alionyesha kushangazwa na kiumbe hicho ambacho anasema
ukubwa wake unamfanya afanane na mnyama mkubwa wa kale aitwaye
dinosaria.
Mark anasema awali alidhani kuwa jina la kisayansi la papa aliyemvua ni
Dactylobatus Clarkii, lakini alipotafuta katika mtandao wa intanet
kuhusiana na samaki wa jamii hiyo alipata taarifa kiduchu.
Hata hivyo, siku chache baadaye, baada ya kuona picha za samaki huyo wa
ajabu, Mtafiti George H. Burgess kutoka Florida Museum of Natural
History alimtambua samaki huyo kuwa ni jamii ya Stingray ambaye jina
lake la kisayansi ni Dasyatis Centroura.
Samaki huyo hupenda kuishi katika kilindi kirefu cha maji katika eneo la
bonde la ufa la baharini huko mashariki mwa Marekani kati ya maeneo la
Carolina na Uruguay, na pia mashariki mwa bahari ya Atlantic.
“Kwa sababu wavuvi wengi hawajihusishi na kuvua katika vina virefu vya
maji ndio maana samaki huyu hajawahi kuonekana mara nyingi. Lakini,
wavuvi wanaotumia meli kubwa pamoja na watafiti wanaofika katika maeneo
ya chini ya bahari wamekuwa wakiwanasa samaki hawa.
“Kwa hakika samaki mkubwa kama huyu anahitaji vifaa maalum vya uvuvi ili
uweze kumuibua hadi juu ya maji. Hawapambani sana wanapokamatwa lakini
ni wazito mno,” anasema.
Mark aliyekuwa akivua huku akipigwa picha na timu ya watengeneza vipindi
vya runinga kutoka Japani, alikuwa ameishusha ndoano yake hadi chini
kabisa ya eneo hilo la maji. Punde, mshipi ulianza kuchezacheza
kuashiria kuwa ndoano ilikuwa imenasa kitu.
“Nilikuwa ninavua kwenye kina cha kama futi 500 hivi na wao walikuwa
wakichukua picha kwa ajili ya kutengeneza kipindi vya televisheni. Kwa
bahati nzuri nikamnasa papa mkubwa mno na kutokana na ukubwa wake
ilituchukua zaidi ya saa nne kumuibua juu ya maji.
Kwanza nikadhani kuwa ni jamii ya papa kwa sababu jinsi alivyokuwa
akipambana wakati wa kumvuta ni kama ambavyo papa anafanya,” anasema
Mark.
Mmoja wa watengeneza filamu hao alikuwa na vifaa vya kupigia mbizi na
alikwenda chini ya maji kurekodi tukio la kukamatwa kwa samaki huyo.
Mark anabainisha kuwa walipomfikisha juu ya maji, watengeneza filamu hao
walimwinua na kumning’iniza kwa dakika kama nne hivi huku wakimpiga
picha na kisha kumuachia. Anaamini kuwa kulingana na ukubwa wake,
alikuwa na uzito unaofikia paundi 800.
No comments:
Post a Comment