Pages

Friday, 3 April 2015

Kwanini Pluto si Sayari?

Kama wewe ni miongoni mwa watu wa rika moja na mimi… Utakumbuka kuwa: Katika somo la Sayansi tulijifunza kuwa Pluto ni sayari ya mwisho katika mfumo wetu wa Jua. Lakini baada ya muda si mrefu ukakoseshwa mtihani kwa kujibu Pluto ni Sayari.
Pengine uliambiwa kwanini Pluto si sayari tena, au pengine mpaka leo ulikuwa unadhani Pluto ni moja ya sayari katika Mfumo wetu wa Jua…
Karibu tuiangalie kwa Undani Historia
ya Pluto kupewa cheo cha U-Sayari, na hatimaye kwa huzuni: Kuvuliwa Cheo hicho:

image
Pluto iligunduliwa kwanza mwaka 1930 na Clyde W. Tombaugh aliyekuwa akifanya kazi katika kituo cha Utafiti cha ‘Lowell Observatory' kilichopo Arizona nchini Marekani.
Of course, hata kabla ya kugunduliwa kwake, wana-Astronomia walikwishabashiri tangu awali kwamba kuna Sayari ya tisa katika mfumo wetu wa Jua. Na kwa vile walikuwa bado hawajaiona, waliipa jina ‘Planet X’.
Siku moja Tombaugh alipokuwa akifanya Kazi aligundua picha moja ya eneo la Anga ilionyesha kitu cha Ukubwa fulani kikiwa kwenye mwendo kama wa Sayari…
Baada ya Uchunguzi zaidi na utafiti wa zaidi ya mwaka mmoja, Tombaugh hatimaye alitangaza kwamba ameigundua ‘Planet X’.
Na kwasababu, yeye na timu yake ndio walifanya Ugunduzi, wakapewa heshima ya kuipa jina Sayari hiyo. Walikuwa na majina mengi, lakini wote wakakubali kuipa jina ‘Pluto’. Jina ambalo kimsingi lilitokana na pendekezo la mtoto wa miaka 11 aliyekuwa akisoma shule Oxford, Uingereza.
Kwa Hiyo baada ya Ugunduzi huo ikawa rasmi kwamba kuna Sayari tisa (9) katika mfumo wetu wa Jua.
Pamoja na Ugunduzi huo, na Uhakiki kwamba Pluto ilikuwepo, wana-Astronomia bado hawakuwa na uhakika wa ukubwa wake.
Mwaka 1978, mwezi wa Pluto uitwao ‘Charon' uligunduliwa. Na kwa kujua Uzito wake, wana-Astronomia wakaweza kujua ukubwa wa Pluto; kwamba ilikuwa na kipenyo (diameter) cha kilomita 2,400.
Ukubwa ambao uliifanya Pluto kuwa Sayari ndogo kuliko zote, ikifuatiwa na Utaridi (Mercury) yenye kipenyo (diameter) cha kilomita 4,880.
Baada ya miaka kadhaa kupita, Teknolojia ikawa imeendelea, na Darubini za kuona Nje ya Anga zikawa zimeboreshwa kiasi cha kuweza kuona vizuri kabisa eneo Pluto ilipo.
Na hapo ndipo mzozo ukaanza… Wana-Sayansi wakagundua kwamba katika eneo Pluto ilipo na kuendelea kulikuwa na magimba mengine, Eneo hili linaitwa ‘Kuiper Belt’.
Wana-Astronomia wanakadiria kuwa kuna magimba kama 70,000 katika eneo hili ambayo yana ukubwa unaoendana na Pluto.
Hii ikawa tatizo, kwani karibu kila Siku gimba jipya likawa linagundulika. Mfano mzuri ni gimba ‘2005 FY9' ambalo linakaribia kidogo kufanana ukubwa na Pluto.
Kwahiyo wana-Astronomia wakajua, muda si mrefu litapatikana gimba jingine ambalo ni kubwa kuliko Pluto…
image
Na kweli, mwaka 2005; Mike Brown na timu yake ya watafiti wakatangaza kwamba wamegundua gimba ambalo ni Kubwa kuzidi Pluto, na kama hiyo haitoshi: Lipo mbali zaidi kuzidi Pluto. Likapewa jina ‘2003 UB313’, ambalo baadaye likaitwa ‘Eris’.
Baada ya ‘Eris' kugundulika, kukatokea mpasuko miongoni mwa wana-Astronomia: Je? 'Eris' nayo ni Sayari… na kama ikiwa Sayari, na magimba mengine maelfu kwa maelfu yaliyogunduliwa nayo pia ni Sayari? kama 'Eris' si Sayari, Kwanini tuiite Pluto sayari?
Maswali kama hayo yaligonga vichwa vya wana-Astronomia wengi, na mijadala mikali ikazuka… Kuna walioipenda Pluto mno kiasi kwamba hawakutata ivuliwe wazfa wa U-Sayari, na wengine waliiona kwamba wakati umefika wa kuuvuliwa wazfa huo.
Basi, wana-Astronomia wote wakakubaliana kwamba uamuzi wa mwisho kuhusu Pluto, na Kuhusu: Ni nini hasa kinacholifanya gimba liwe Sayari ungefikiwa katika Mkutano mkuu wa ishirini na sita (26) wa Umoja wa kimataifa wa wanaastronomia Duniani (Internationa Astronomical Union) uliofanyika tarehe Agosti 14 mpaka Agosti 25, 2006 jijini Prague.
Wana-Astronomia katika Umoja huo wakapewa nafasi ya kupiga kura juu ya ‘Maana ya Sayari’. Kulikuwa na machaguo (option) matatu (3) na walitakiwa kuchagua moja.
Kama Chaguo la kwanza lingepita ingemaanisha: Kungekuwa na Sayari 12. Pluto ingebaki kuwa Sayari, lakini pia ‘Eres’, na hata ‘Ceres' ambayo awali ilikuwa kwenye kundi la Asteroidi.
Kama Chaguo la Pili lingepita ingemaanisha: Tungebakiwa na Sayari tisa (Pluto ikiwemo), na Hakuna Sayari nyingine ambayo ingeongezwa TENA.
Chaguo La Tatu lilimaanisha: Pluto ingevuliwa wazfa wa kuwa Sayari, na tungebakiwa na Sayari nane. Lakini pia lilimaanisha: Kama Pluto si sayari tena; Imekuwa kitu gani?
Kura zikapigwa; Na Chaguo La Tatu Likapita! Pluto ikavuliwa madaraka ya U-Sayari, na tukabakiwa na Sayari nane.
Lakini pia, Kundi jipya la magimba likaundwa. Kundi hili linaitwa SAYARI KIBETE (DWARF PLANET). Basi, Pluto pamoja na rafiki yake mpya ‘Eris' wakatupiwa kwenye kundi hilo.
Kama unakumbuka, nilikwambia katika mkutano huu pia wakakubaliana rasmi, Nini haswa maana ya Sayari.
Wakasema, Ili Gimba liweze kuitwa Sayari linabidi liweze kukidhi masharti matatu, Ambayo ni:
  1. Linabidi liwe Gimba linalozunguka Jua
  2. Ukubwa wake unasababisha graviti ya Kutosha ili kulazimisha mada (mass) yake kuchukua umbo kama mpira (spherical shape).
  3. Katika njia (orbit) ambalo linazunguka linabidi liwe kubwa kiasi kwamba limesafisha njia kwa kuvuta (attract) kwake magimba mengine madogo yaliyo karibu.
Kwahiyo, kwa mashariti na vigezo hivyo, Pluto ikawa imefaulu kigezo namba moja na mbili, lakini ikawa imefeli namba tatu.
Magimba yote ambayo yanafaulu namba moja, na namba mbili lakini si tatu, yanaitwa Sayari Vibete (Dwarf Planets)
Mfumo wetu wa Jua una Sayari vibete tano mpaka sasa, Kuna: Pluto, ‘Eris’, ‘Ceres’, ‘Haumea' na 'Makemake’.
image
Pamoja na kuvuliwa madaraka, Pluto bado huvuta hisia nyingi kwa wana-Astronomia mbalimbali, na bado ni mahali panapoleta hamasa ya kwenda kutafita, na hatimaye hata kufika siku moja.
Na bado, hata leo wapo watu wengi ambao bado wana Huzuni juu ya namna Pluto ilivyovuliwa madaraka…
like page yetu kwa habari zaidi

No comments:

Post a Comment

 

Blogger news

Blogroll

LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZA KILA WAKATI

Receive all updates via Facebook. Just Click the Like Button Below

Powered By Blogger Widgets