TWAHITAJI kuelewa kindani kidogo
jinsi ambavyo dunia imeumbwa ili tuweze kuelewa mambo yaliyoonwa na
watafiti waliokuwa kwenye chombo cha Alvin. Yaaminika kuwa dunia yetu imefanyizwa na tabaka thabiti (linaloitwa lithosphere)
linalokalia mwamba ulioyeyuka, unaosogea polepole. Kwa wazi, tabaka
thabiti la nje lina kina cha takriban kilometa 100 nalo hufanyiza
asilimia 0.6 hivi tu ya dunia yote. Tabaka la nje kabisa, si laini, ni
nene mno chini ya mabara na jembamba kiasi cha kilometa sita chini ya
safu ya milima iliyo katikati ya bahari.
Isitoshe, tabaka hilo thabiti la nje
si zima kama ganda la yai, bali limegawanyika. Badala yake, laonekana
likiwa limegawanyika katika mabamba kadhaa makubwa yaliyo thabiti, na
mengine mengi madogo, yote huitwa miamba mikuu (tectonic plates).
Miamba hiyo hufanyiza mabara na mabonde ya bahari. Miamba hiyo
husogea-sogea. Mahali inapotengana, inaacha pengo na kutokeza nyufa
katika safu ya milima ya katikati ya bahari. Ulimwenguni pote, miamba
hiyo husogea kwa mwendo wa wastani wa sentimeta tatu hivi kwa mwaka.
Kulingana na nadharia ya miamba ya
dunia, kadiri miamba inavyotengana karibu na safu ya milima ya katikati
ya bahari, ndivyo inavyoruhusu miamba moto iliyo katika tabaka la
katikati la dunia, chini tu ya tabaka la juu, ipande. Myeyuko huo moto
hufanyiza tabaka jipya baharini katikati ya miamba mikuu miwili, lakini
miamba hiyo haiungani. Badala yake, inasukumwa mbali zaidi, na hilo hufanya safu ya milima ishabihi kidonda kikubwa kisichopona.
Wakati matabaka mapya yanapofanyizwa
kwenye mwamba mkuu katika safu ya milima iliyo katikati ya bahari,
upande mwingine wa mwamba huo hushuka polepole chini ya mwamba mkuu
jirani na kutumbukia katika tabaka la katikati lililo moto. Huyeyushwa
na kuwa sehemu ya tabaka hilo. Mahali ambapo mwamba mkuu husukumwa chini
huitwa eneo la mshuko (subduction zone). Maeneo ya mshuko huwa
na mojawapo ya mabonde yenye kina zaidi ulimwenguni. Kwa mfano, Bonde
la Mariana lililo karibu na pwani ya Guam katika Bahari ya Pasifiki,
lina kina cha zaidi ya meta 11,000. Kama Mlima Everest, ulio mrefu zaidi
duniani ungewekwa kwenye bonde hilo, kilele chake kingekuwa meta 2,000
chini ya maji!
Chemchemi—Yenye Sumu!
Kwa sababu ya hali yake ya
kubadilika-badilika na milipuko ya volkano, safu ya milima ya katikati
ya bahari ina vijito tele vya volkano na matundu mengi ya maji moto.
Mchanganyiko moto sana wenye sumu wa maji na madini ya ardhini
hububujika kutoka kwenye matundu hayo. Lakini, jambo la kushangaza ni
kwamba mazingira hayo yasiyokalika, yanayokumbwa na kanieneo zinazozidi
kwa mbali sana zile zilizo katika usawa wa bahari, huvutia viumbe chungu
nzima—badala ya kuvifukuza! Mamia ya jamii za viumbe wanaoishi humo
zatia ndani bakteria, chaza wakubwa—wenye urefu wa thuluthi ya meta
hivi—na, la kuduwaza zaidi, choo aina ya tube worm wenye minyiri-minyiri ya rangi nyekundu iliyoiva wanaojishikilia kwa nguvu kwenye sakafu ya bahari na kufikia kimo cha meta 1.8.
Viumbe wanaoishi katika matundu ya
baharini huvunda kama mayai yaliyooza wanapoletwa ufuoni! Uvundo huo
hausababishwi na kuoza, bali na hidrojeni salfaidi—kemikali yenye sumu
kali inayotoa uvundo wenye kuchukiza ambayo imejaa kote katika matundu
ya maji moto. Maji yanayotoka katika matundu hayo yana asidi kali na
metali nyingi, kutia ndani shaba, magnesi, chuma, na zinki. Badala tu ya
kustahimili katika mazingira hayo—ambayo yamelinganishwa na mahali pa
kutupa takataka zenye sumu—tube worm na viumbe wengine husitawi humo! Jinsi gani? Ili kuelewa, acheni tumchunguze tube worm kinaganaga.
Kiumbe Asiyeeleweka
Wanabiolojia walipowachunguza tube worm, waligundua
kwamba ni viumbe wasioeleweka. Hawakuwa na kinywa wala mfumo wa
umeng’enyaji. Swali likazuka, Wao hulaje na kufyonza chakula chao? Kisha
wakagundua jambo lenye kuduwaza: Choo hao walikuwa na damu nyekundu—si
umajimaji tu bali damu halisi, yenye himoglobini nyingi—inayozunguka
katika mwili wao na katika minyiri-minyiri yao inayoshabihi manyoya.
Mafumbo hayo yalizidi kuwa tata wakati wanabiolojia walipopasua kifuko cha ute katika mwili wa tube worm. Tishu
zake zilikuwa na mchanganyiko wa bakteria zipatazo bilioni 10 kwa kila
gramu ya tishu! Mnamo mwaka wa 1980 mwanafunzi mmoja wa biolojia alibuni
nadharia ya kwamba tube worm huishi kwa utegemeano—utegemeano
huwawezesha viumbe wawili kupata manufaa kwa kushirikiana. Utafiti
ulithibitisha nadharia yake kwa kuonyesha kwamba tube worm, akiwa kimelewa, hulisha bakteria hizo, na bakteria humlisha.
Kama mashavu ya samaki, minyiri-minyiri ya tube worm hukusanya
oksijeni na kaboni, vitu vinavyotumiwa na bakteria kutengenezea
chakula. Minyiri-minyiri hiyo haipeperuki moja kwa moja kwenye maji moto
yanayomiminwa na matundu—kufanya hivyo kungekuwa kuhatarisha uhai—bali
hupeperuka katika sehemu ambako maji moto ya matundu huchanganyika na
maji baridi sana ya baharini. Bila shaka, utengenezaji huo wa chakula
huhitaji nishati. Katika uso wa dunia—na juu-juu ya bahari—nuru ya jua
huandaa nishati muhimu kwa utengenezaji wa chakula kwa kusababisha ukuzi
wa mimea. Lakini nuru ya jua haifiki hata kidogo katika lindi kuu
anamoishi tube worm.
Nishati Kutoka Katika Kiini cha Dunia
Kwa akili nyingi, Muumba ameandaa
nishati inayohitajiwa kutoka kwa kiini cha dunia kupitia kwa matundu ya
maji moto na ile kemikali yenye uvundo ya hidrojeni salfaidi. Hidrojeni
salfaidi ambayo ni “nuru ya jua” ya jamii zinazoishi katika matundu ya
baharini, huandaa nishati inayohitajiwa na bakteria katika utengenezaji
wa chakula. Wakati huohuo, bakteria hizo ni kama “mimea” katika jamii
zinazoishi kwenye matundu kwa sababu ndizo za kwanza katika mlishano wa
viumbe wanaoishi katika matundu ya baharini.*
Ili kuweza kuchanganya kemikali zote zinazohitajiwa na bakteria, damu ya tube worm ina
molekuli za himoglobini ambazo ni kubwa mara 30 zaidi ya molekuli za
himoglobini katika mwili wa mwanadamu. Damu husafirisha kemikali hizo
kwa bakteria zenye njaa, kisha bakteria humtengenezea tube worm chakula.
Uhai Katika Matundu—Viumbe Mbalimbali!
Kwa kweli, hakuna kiumbe yeyote
anayeishi katika matundu hayo anayepasa kufa njaa, kwa kuwa bakteria
zimezagaa kotekote—nyakati nyingine hufanyiza rundo kubwa! Hata katika
maji vuguvugu yanayobubujika kwa nguvu juu ya matundu, nyakati nyingine
bakteria hukusanyika kwa wingi, mfano wa dhoruba ya theluji, na
kufanyiza mfano wa supu iliyo hai. Wanyama wengine hufurahia pia
utegemeano pamoja na bakteria hao sawa na tube worm, ilhali
wengine hula vijiumbe hao moja kwa moja. Kwa kweli, viumbe wanaoishi
karibu na matundu ya baharini wanasitawi na kunawiri sana hivi kwamba
wamelinganishwa na vinamasi vya maji ya chumvi, misitu ya kitropiki ya
mvua, na matumbawe katika maji yasiyo na kina.
Kwa kweli, jamii mpya 300 tayari
zimegunduliwa karibu na matundu hayo. Hizo zatia ndani chaza weupe
wakubwa na kome (rangi si lazima katika mazingira yenye giza totoro),
pweza, na kaa weupe walafi wanaopenda mno kula minyiri-minyiri
mitepetevu ya tube worm. Ili kujilinda, tube worm huwa na tendo-hiari la haraka ambalo huficha mara moja minyiri-minyiri hiyo ndani ya mwili wake.
Viumbe wengine wanaoishi katika
matundu hayo watia ndani buibui wa baharini, konokono, uduvi wenye
kucheza-cheza, koanata, na wanyama wenye magamba, samaki wanaofanana na
mkunga ambao hunyiririka kwenye miamba iliyofunikwa na bakteria na
salfa, tube worm wadogo na choo wengine. Hao choo wengine hutia
ndani choo wa tambi na choo wa chwago. Choo wa tambi wana jina
linalofaa kwa sababu wanashabihi tambi nyeupe nyingi zinazoning’inia
kwenye miamba. Choo wa chwago ni wa pekee kwa sababu wanaweza
kustahimili joto kali kufikia nyuzi Selsiasi 80! Bila shaka, bakteria wa
matunduni, ambao huishi kwenye choo wa chwago, wanaweza pia kustahimili
joto kali.*
Nuru ya Ajabu!
Mnamo mwaka wa 1985, wanasayansi
walishangaa kuona uduvi wenye sehemu mbili zinazoshabihi macho wakiwa
karibu na matundu ya baharini, sehemu hizo zisizo na lenzi zina kemikali
zinazotambua nuru kwa wepesi. Bila shaka, swali walilofikiria kwanza
ni, Wanyama hao wanaweza kuona nini katika giza totoro? Ili kupata
jawabu, watafiti walitumia kamera ya tarakimu yenye nguvu sana, kama ile
inayotumiwa kupiga picha nyota hafifu sana. Waliielekeza kamera hiyo penye tundu, wakazima taa zote, kisha wakapiga picha.
Matokeo yalishangaza. Picha kwenye
kompyuta ilifunua “nuru maridadi, dhahiri na yenye kung’aa” ukingoni mwa
bomba yalimotokea maji moto, asema mwanasayansi Cindy Lee Van Dover.
Je, uduvi hutumia nuru hii ya ajabu, isiyoweza kuonwa kwa macho ya
mwanadamu? Vyovyote iwavyo, ugunduzi wa kwamba matundu ya maji moto
hutoa nuru “waanzisha fani mpya kabisa ya utafiti,” aongezea Van Dover.
Mkubwa Zaidi na Mdogo Zaidi
Hivi majuzi, sehemu ya sakafu ya
bahari iliyojaa methani, iligunduliwa kuwa makao ya bakteria mkubwa
zaidi aliyewahi kugunduliwa katika sayansi. Majitu hayo yaliyogunduliwa
mwaka wa 1997, yanashabihi ushanga yakiwa na urefu unaozidi ule wa
bakteria za kawaida kwa mara 100 hadi 200. Wao pia hula kupindukia, hula
karibu salfaidi yote yenye sumu iliyo kwenye tope, na hivyo hufanya
eneo hilo kuwa salama kwa viumbe wengine wa baharini.
Kiumbe anayedhaniwa kuwa mdogo zaidi duniani aligunduliwa hivi karibuni pia chini ya bahari, lakini umbali wa kilometa tano ndani ya sakafu ya bahari! Ripoti moja katika gazeti la The New York Times yaeleza
ugunduzi huo, uliotukia karibu na ufuo ulio Magharibi mwa Australia,
kuwa “wa ajabu sana kiasi cha kuzusha mjadala mkali ulimwenguni pote.”
Swala linalobishaniwa ni kama nanobe—zinaitwa hivyo kwa sababu
hupimwa ukubwa kwa nanometa, au kipimo cha sehemu moja kwa bilioni ya
meta—ni viumbe au la. Hufanana na kuvu, hutoshana na virusi, vina DNA,
na yaonekana huzaana upesi na kufanyiza makundi makubwa.
Viumbe wengi wanagunduliwa sasa,
hivi kwamba wanasayansi wanaamini kuwa idadi ya vijiumbe vilivyo ndani
ya tabaka la juu la dunia yaweza kuzidi idadi ya vijiumbe vilivyo kwenye
uso wa dunia! Ugunduzi huo unaleta mabadiliko katika dhana za
kisayansi. Mwanasayansi mmoja alisema: “Tumetupilia mbali ushikiliaji wa
kauli katika elimu ya vijiumbe katika miaka kadhaa iliyopita. Fani hiyo
imepiga hatua madhubuti. Kwa kweli ni sayansi mpya.”
Isitoshe, ugunduzi huo wenye kina
watufundisha somo fulani linalozidi sayansi. Biblia yaeleza waziwazi
somo hilo: “Sifa zake [Mungu] zisizoonekana zaonwa waziwazi tangu
uumbaji wa ulimwengu na kuendelea, kwa sababu zafahamiwa kwa vitu
vilivyofanywa.” (Waroma 1:20)
Mathalani, Mungu anahangaikia sana usafi. Hilo lathibitishwa na
bakteria na viumbe wengine wa baharini wanaoondoa sumu hatari zinazotoka
ndani ya dunia na kutoka kwa vitu vingine vinavyozama na kuoza kutoka
sehemu ya juu ya bahari. Kwa wazi, Mungu anahangaikia hali-njema ya
sayari yetu na viumbe wote waliomo. Kama tutakavyoona katika makala
ifuatayo, sifa hiyo ya Muumba yahakikisha kuwapo kwa wakati ujao mtukufu
kwa ajili ya viumbe wote duniani.
[Maelezo ya Chini]
Bakteria zinazoishi
katika matundu ya baharini hutumia utaratibu unaoitwa usanidi-kemia.
Neno hilo latofautiana na usanidi-nuru, utaratibu unaotegemea nishati ya
jua unaotumiwa na mimea iliyo ardhini na fitoplankitoni. Fitoplankitoni
yatia ndani mimea au viumbe vinavyofanana na mimea vinavyoelea katika
sehemu ya juu ya bahari, inayopata nuru ya jua.
Katika miaka ya
1960, wanasayansi walianza kuchunguza bakteria wanaopenda joto
waliopatikana katika chemchemi za maji moto katika Mbuga ya Taifa ya
Yellowstone huko Marekani. Kwa sababu ya “mazingira yenye hali ngumu
sana ya jamii hizo za viumbe” ambayo yanastaajabisha, chasema kitabu cha
The Deep Hot Biosphere, “wanasayansi walifahamu kwa mara ya kwanza sifa za kipekee za viumbe walioko duniani wanaoonekana kuwa sahili zaidi.”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Matundu ya Maji Moto Ni Nini?
Katika safu ya milima ya volkano
iliyo katikati ya bahari, maji ya bahari hupenya nyufa zilizo katika
tabaka la juu la dunia na kuingia katika maeneo yenye joto kali
kupindukia. Maji hayo huchemka kabisa, kisha hufyonza kemikali kadhaa
yanapopenya miamba. Pia husukasuka, na kufika kwenye sakafu ya bahari,
na hivyo hufanyiza matundu ya maji moto—chemchemi za maji moto.
Chemchemi hizo “bila shaka zina nguvu na huvutia sana kama chemchemi
zilizo ardhini,” chasema kichapo kimoja.
Isitoshe, joto la chemchemi hizo
zilizo kwenye sakafu ya bahari laweza kufikia nyuzi Selsiasi 400, moto
zaidi kushinda risasi iliyoyeyuka! Lakini kwa sababu ya kanieneo ya
bahari iliyo juu, kioevu hicho chenye joto sana hakiwi mvuke. Jambo la
kushangaza ni kwamba milimeta chache tu kutoka kwa mkondo wa maji moto,
kwa kawaida joto la wastani la bahari huwa nyuzi Selsiasi moja au mbili
tu kushinda barafu. Madini yanayotoka kwa maji hayo moto yanayopoa upesi
hujikusanya kwenye sakafu ya bahari, ambapo yanafanyiza vilima na
mabomba. Mabomba hayo yaweza kuwa na kimo cha meta tisa. Kwa kweli,
bomba moja lenye kimo cha meta 45 na kipenyo cha meta 10 hivi
liligunduliwa, na bado lilikuwa likirefuka!
Matundu ya maji moto yanaweza
kububujika na kutulia ghafula, na hilo ni hatari sana kwa viumbe
wanaoishi karibu na matundu hayo. Hata hivyo, viumbe fulani huepuka
hatari kwa kuhamia kwenye matundu mengine.
No comments:
Post a Comment