Dar es Salaam.
Mahakama ya Rufani imetupilia mbali
maombi ya marejeo kuhusu uhalali wa uamuzi wa Mahakama Kuu Dar es Salaam
kuwafutia mashtaka ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare na mwenzake
Joseph Ludovick Rwezahura.
Hatua hiyo ya mahakama imefanya kiongozi
huyo wa Chadema na mwenzake kuibwaga Serikali kwa mara ya pili
mahakamani katika mashitaka dhidi yao.
Maombi hayo namba 5 ya mwaka
2014, yalifunguliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) katika Mahakama ya
Rufani akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kufumfutia
mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu.
Uamuzi wa kutupilia mbali maombi hayo ulisomwa jana na
Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Zahra Maruma kwa niaba ya Jopo la
Majaji watatu wa mahakama hiyo lililokuwa limepangwa kusikiliza maombi
hayo.
Majaji hao ni Nathalia Kimaro (kiongozi wa jopo), William Mandia na Profesa Ibrahimu Juma.
Mahakama
hiyo ilifikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa maombi hayo
yalikuwa na dosari za kisheria kutokana na DPP kutoambatanisha mwenendo
wa uamuzi wa Mahakama Kuu aliokuwa akiupinga.
Dosari hiyo iliibuliwa
na Jaji Prosefa Juma katika tarehe ambayo maombi hayo yalikuwa
yamepangwa kusikilizwa ambapo alihoji iwapo ni halali kusikiliza maombi
hayo bila kuwepo kwa mwenendo huo.
Wakili wa Serikali Mwandamizi,
Angaza Mwipopo akisaidiana na Wakili Serikali Mwandamizi, Hashim Ngole,
alijibu kuwa wanachopinga ni uamuzi wa mahakama kufuta mashtaka katika
kesi ambayo haikuwa mbele yake.
Wakili Angaza alidai kwamba
kutokuwepo kwa mwenendo huo hakuathiri na kwamba mahakama ina uwezo wa
kuyasikiliza maombi hayo hata bila kuwepo kwa mwenendo huo.
Akijibu
hoja hizo, Wakili wa Lwakatare, Peter Kibatala alisema kuwa suala la
mwenendo wa uamuzi unaopingwa ni miongoni mwa hoja za pingamizi lake la
awali dhidi ya maombi hayo.
Wakili Kibatala alidai kuwa kutokuwepo
kwa mwenendo huo ni dosari ambayo ina athari kubwa kiasi kwamba mahakama
haitakuwa na uwezo wa kutoa kile kinachoombwa.
Alisisitiza kuwa kutokuwepo kwa kumbukumbu za mwenendo huo ni athari ambayo tiba yake ni mahakama kuyatupilia mbali maombi hayo.
Wakili
Mwipopo alisisitiza kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 65 ya Kanuni za
Mahakama ya Rufani, siyo lazima kuambatanisha mwenendo katika maombi na
kwamba nyaraka za msingi kwa mujibu wa kanuni hiyo ni hati ya kiapo,
ambavyo wameviambatanisha.
Hata hivyo, kupitia uamuzi wake jana,
mahakama ilisema kuwa msimamo wa kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 4
(3) cha Sheria ya Mamlaka ya Mahakama ya Rufani ni lazima kuambatanisha
mwenendo wa uamuzi unaopingwa, uamuzi na amri ya mahakama katika maombi
ya marejeo.
“Kutokana na kasoro hiyo ya kutokuwepo kwa mwenendo wa
uamuzi unaopingwa, tunatupilia mbali maombi haya,” ilisema mahakama
katika uamuzi wake.
Katika maombi hayo, DPP alikuwa akiiomba Mahakama
ya Rufani iitishe majalada ya kesi hiyo na kuchunguza uhalali wa uamuzi
wa Mahakama Kuu kuwafutia washtakiwa hao mashtaka ya ugaidi na kisha
ifute uamuzi huo wa Mahakama Kuu na amri zote ilizozitoa. Pamoja na
mambo mengine, DPP alikuwa akidai kuwa haikuwa sahihi Mahakama Kuu
kuamua kuwa mashtaka hayo hayakuwa halali, kwani hapakuwa na taarifa
zilizowasilishwa dhidi ya washtakiwa, ambazo Mahakama Kuu ingezizingatia
katika kuamua uhalali wake.
Kulingana na uamuzi huo, DPP anaweza
kufungua tena maombi hayo baada ya kurekebisha kasoro hiyo, lakini baada
ya kuomba kibali cha mahakama kufungua marejeo hayo nje ya muda wa
kawaida kisheria.
Akizungumzia kesi hiyo, Lwakatare alisema: “Kwanza
namshukuru sana Mungu kwa kuniwezesha kushinda kesi hii…; kusema kweli
ilikuwa kesi ngumu na mbaya, hasa ikizingatiwa kwamba ilikuwa ndiyo kesi
ya kwanza ya ugaidi kufunguliwa hapa nchini.”
Lwakatare aliongeza:
“Nawashukuru mawakili wangu ambao wamekuwa wakisimamia kesi hii pamoja
na makahama pia kwa kutenda haki leo (jana). Kama ungefanyika uamuzi
tofauti na huu, basi ningebaki Segerea. Pia, haki hiyo imeweza kutendeka
kutokana na misingi ya kesi husika kuwa ya kusuasua. Kesi ilifunguliwa
kwa jabza na shinikizo la kisiasa.”
Alieleza kuwa, licha ya shinikizo hilo, haki imeweza kutawala na ameshinda kesi hiyo mbali na misukusuko aliyopitia.
Alisema
kwamba anatumaini makahama itaendelea kutoa hati katika kutoa uamuzi wa
kesi yake iliyobaki katika Makahama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Naye Wakili Kibatala alisema kuwa kwa hali ilivyo suala hilo limekwisha na kwamba DPP hana mwanya wa kurudi tena na maombi hayo.
Alifafanua
kuwa kwa kawaida maombi ya marejeo hufunguliwa katika muda wa siku 60
tangu siku ya kutolewa kwa uamuzi unaopingwa na kwamba, nje ya muda huo
mwombaji analazimika kuomba kibali cha Mahakama kufungua maombi nje ya
muda na kutoa sababu za kuridhisha.
“Siku 60 tayari zimeshakwisha,
hivyo DPP akitaka kurudi tena ni lazima aombe kibali na atoe sababu za
kuiridhisha Mahakama. Sababu za kuridhisha ni pamoja na ugonjwa, au
kuchelewa kupata nakala ya uamuzi na mwenendo kutoka mahakamani, lakini
siyo kwa uzembe,” alisema.
Lwakatare na Ludovick walikuwa
wakikabiliwa na mashtaka manne, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
matatu kati yake yakiwa ya ugaidi na moja la kawaida la jinai.
Mashtaka
hayo ya ugaidi yalikuwa ni kupanga kumteka aliyekuwa Mhariri Mtendaji
wa Gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky na kisha kumdhuru kwa sumu,
kushiriki mkutano wa vitendo vya ugaidi (kwa washtakiwa wote) na
kuhamasisha vitendo vya ugaidi lililokuwa likimkabili Lwakatare pekee.
Shtaka
lingine la jinai lilikuwa ni kula njama ya kutenda makosa, ambalo
lilikuwa likiwakabili wote kwa pamoja na bado linaendelea katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hata hivyo, Mei 8, mwaka huu Jaji
Lawrence Kaduri wa Mahakama Kuu aliwafutia mashtaka ya ugaidi, baada ya
mawakili wa Lwakatare kufungua maombi wakipinga uamuzi wa DPP kuwafutia
mashtaka katika kesi ya awali na kisha kuwakamata na kuwafungulia
mashtaka hayohayo.